Mukwege, Murad wakabidhiwa tuzo ya Nobel
10 Desemba 2018Katika sherehe za kusisimua zilizohudhuriwa na familia ya kifalme na wageni mia kadhaa wa hishma, mwenyekiti wa kamati ya Nobel, bibi Berit Reiss-Anderssen amewasifu washindi hao wawili, Nadia Murad mwenye umri wa miaka 25 na tabiibu Denis Mukwege mwenye umri wa miaka 63 na kuwataja kuwa "Sauti yenye nguvu ya dunia katika ulimwengu wa leo."Mapambano ya kuania haki yamewaleta pamoja licha ya maeneo tofauti walikotokea.
Bibi Berit Reiss-Andersen ameendelea kusema:"Washindi wote wawili wanataka maovu yaandamwe kisheria, uhalifu wa vita lazma uadhibiwe na kwamba jukumu lisalie mabegani mwa jumuia ya kimataifa. Wote wawili wanastahiki kikamilifu tuzo ya amani ya Nobel."
Jumuia ya kimataifa inabidi iwe macho
Akitoa shukurani zake, daktari huyo wa maradhi ya wanawake Denis Mukwege amesema vita pekee vinabidi viwe vita dhidi ya hali ya watu kutojali" na kuitolea wito jumuia ya kimataifa wasiyafumbie macho matumizi ya nguvu ya kingono katika maeneo ya mizozo.
Mukwege ambae juhudi zake katika eneo la mashariki mwa jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo zimempatia sifa za shujaa anaepambana na ubakaji kama silaha ya vita ameitolea wito jumuia ya kimataifa ijiunge nao katika kukomesha madhila yanayoutia aibu ubinaadamu.
Ulinzi wa wayazid ni jukumu la jumuia ya kimataifa
Kwa upande wake Nadia Murad akishangiriwa miongononi mwa wengineo na mwanaharakati wa haki za binaadam, muingereza mwenye asili ya Libnan, Amal Clooney amewasihi walimwengu wailinde jamii yake ya Yazid."Ulinzi wa wayazid ni jukumu la jumuia ya kimataifa na taasisi za kimataifa" amesema na kusisitiza "bila ya ulinzi wa kimataifa, hakuna kitakachowahakikishia kama hawatokabiliawa tena na balaa la mauwaji kutoka makundi mengine ya kigaidi".
Mbali na tuzo ya amani ya Nobel, tuzo nyengine za Nobel zimetolewa leo hii pia lakini mjini Stockholm, isipokuwa ile ya fasihi iliyoakhirishwa hadi mwaka 2019. Tuzo ya amani ya Nobel ni mchanganyiko wa nishani ya dhahabu, shahada na hundi ya safaru ya Sweeden Crone milioni tisa ambayo ni sawa na Euro 871.000-
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/AFP/
Mhariri:Yusuf Saumu