Mzozo kati ya Ufaransa na Australia hautazuia mkataba
20 Septemba 2021Balozi wa Ufaransa nchini Australia Jean-pierre Thebault amekanusha ripoti za vyombo vya habari kwamba taifa lake linaushinikiza Umoja wa Ulaya kutosaini mkataba huo wa kibiashara na Australia ambao umekuwa ukijadiliwa tangu mwaka 2018. Thebault ameliambia shirika la utangazaji nchini Australia kwamba kufikia sasa, mashauriano yanaendelea na kuna shauku kubwa kwa Australia kuwa na mkataba huria wa kibiashara na Umoja wa Ulaya akiongeza kwamba mkataba kama huo una uwezo wa kuleta manufaa makubwa kwa Australia.
Waziri wa biashara wa Australia Dan Tehan amesema atasafiri kuelekea Uingereza katikati ya wiki hii kwa mazungumzo ya kibiashara na ana azma kubwa ya kukutana na mwenzake wa Ufaransa Franck Riester. Akizungumzia kuhusu ziara yake ya mwezi Aprili, Tehan amesema ana uelewa mkubwa kuhusu ziara hiyo barani Ulaya kuzungumzia mkataba huo wa biashara huria na Umoja wa Ulaya na kwamba ni kwa maslahi ya pande zote mbili za Australia na Umoja huo. Tehan ameongeza kwamba haoni sababu kwanini mazungumzo hayo hayapaswi kuendelea.
Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya imesema inatathmini mkataba wa kijeshi kati ya mataifa matatu ya Marekani, Uingereza na Australia. Haya yanajiri wakati ambapo Rais wa Ufaransa Emmanuel Macro anatarajiwa kufanya mkutano na rais wa Marekani Joe Biden katika siku chache zijazo katika mkutano wao wa kwanza wa ana kwa ana tangu kuzuka kwa mzozo huo wa kidiplomasia.
Ufaransa yawaondoa mabalozi wake Marekani na Australia
Ufaransa iliwaondoa mabalozi wake Marekani na Australia na kuwarejesha nyumbani baada ya rais Joe Biden kufichua wiki iliyopita kwamba muungano mpya wa mataifa matatu yanayoijumuisha Australia na Uingereza utaiwezesha Australia kupata nyambizi angalau nane zenye uwezo wa nyuklia. Mkataba huo umesababisha kufutwa kwa makubaliano ya dola bilioni 66 kati ya Australia na Ufaransa ambapo kampuni ya manowari ya serikali ya Ufaransa ilikuwa itengenezee Australia nyambizi 12 za kawaida. Pesa hizo zingetumika kwa zaidi ya miaka 35.
Wakati huohuo, mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya, Jumatatu (21.09.2021) watakutana pembezoni mwa kongamano kuu la baraza la Umoja wa Mataifa kuzungumzia kuhusu mkataba huo mpya kati ya mataifa hayo matatu ya Australia, Marekani na Uingereza AUKUS. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Umoja wa Ulaya Peter Stano amesema kuwa hiyo ni fursa ya kwanza wa mawaziri hao kuzungumzia athari za mkataba huo na kuongeza kuwa mkutano huo ni fursa ya kuzungumzia sio tu masuala kati ya Ufaransa na Australia lakini athari jumla za muungano huo wa AUKUS.