Nani anayeweza kuleta amani Libya?
30 Desemba 2019Rais Recep Tayyip Erdogan atafanikiwa, kama bunge la Uturuki litaidhinisha mpango wake katika siku chache zijazo. Erdogan anataka kutoa msaada wa kijeshi kwa serikali ya Tripoli inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa katika vita vyake dhidi ya mbabe wa kivita Khalifa Haftar.
Tangu kuangushwa kwa aliyekuwa kiongozi wa muda mrefu Muammar Gaddafi mwaka wa 2011, mazingira yamekuwa yenye vurugu. Serikali mbili pinzani ziliibuka: serikali ya Fayez al Sarradj mjini Tripoli, ambayo inatambulika na mataifa mengi na Umoja wa Mataifa, na wapinagaji wa Jenerali Khalifa Haftar anayedhibiti mashariki mwa nchi hiyo na anaungwa mkono na Misri, Umoja wa Falme za Kiarabu na Urusi miongoni mwa wengine.
Wanajeshi wa Haftar wa Libyan National Army walianzisha operesheni ya kuishambulia Tripoli mwezi Aprili. Serikali ya Sarraj ikaonekana kuzidiwa nguvu. Mnamo Novemba, Sarraj alisaini makubaliano na Uturuki, ambayo yanairuhusu serikali ya Ankara kutuma wanajeshi wa angani, ardhini na wanamaji na kupeleka silaha. Claudia Gazzini kutoka shirika la kimataifa la International Crisis Group anasema ilibidi Saraj akubali msaada wa Uturuki lakini hiyo ina maana kuwa vita vya kuudhibiti mji mkuu vitaongezeka.
Umoja wa Ulaya unajaribu kusimamia mpango wa kusitishwa vita nchini Libya. Hata hivyo kwa mujibu wa mtalaamu Gazzini, kongamano lililopangwa kuandaliwa Berlin Januari mwakani halina nafasi kubwa ya kufanikiwa.
Gazzini, ambaye alifanya kazi kama mshauri wa mjumbe maalum wa Umoja wa Mataiafa nchini Libya Ghassan Salame, amesema Jenerali Haftar hayuko tayari kufanya mazungumzo na anataka kunyakua madaraka kwa gharama yoyote ile. Mbabe huyo anataka kuendeleza vita na atafanya hivyo mradi tu anapata msaada wa kijeshi kutoka kwa washirika wake.
Kando na hayo, mataifa ya Ulaya hayana msimamo wa pamoja katika mzozo wa Libya. Mchambuzi wa masuala ya kisiasa nchini Libya Mohamed Fouad natarajii jukumu lolote muhimu kutoka Ulaya.
Kimataifa, ushirikiano wa kijeshi kati ya serikali ya Sarraj na Uturuki ni wenye utata mkubwa. Utruruki pia imesaini makubaliano na serikali ya Tripoli kudhibiti mpaka wa bahari ya Mediterania. Gazzini anasema mataifa ya Ulaya yanaiona hatua hiyo kuwa ukiukaji wa sheria ya Ugiriki. Na Ulaya ina mashaka kuhusu ushirikiano huo.
Kwa Erdogan hata hivyo, Libya inaonekana kuwa uwanja mwingine ambao inaweza kupigana na Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu na Misri – wote wakiwa ni washirika wa Haftar – kwa udhibiti wa kanda hiyo.