Neno "Nafri" laiweka pabaya polisi ya Ujerumani
2 Januari 2017Suala hili limekuja juu baada ya polisi katika mji wa Cologne kutuma ujumbe wa Twitter juu ya juhudi za kudhibiti watu wanaohudhuria mikusanyiko ya sherehe.
"Mamia ya Wanafri wanakaguliwa hivi sasa kwenye kituo kikuu cha treni," ulisema ujumbe wa Twitter wa polisi katika sherehe za Mkesha wa Mwaka Mpya usiku wa kuamkia Jumapili mjini Cologne.
Nafri ni neno linalotumiwa na polisi kumaanisha "Wahalifu kutoka Afrika Kaskazini". Mamlaka nchini Ujerumani ziliongeza idadi ya maafisa wa polisi kufuatia mkasa wa Mkesha wa Mwaka Mpya 2016 kwenye mji huo, ambapo mamia ya wanawaek walifungua malalamiko kwamba walishambuliwa kijinsia na kuibiwa vitu vyao na makundi makubwa ya wageni. Maafisa wanaamini wengi wa waliofanya makosa hayo walikuwa na asili ya Afrika Kaskazini.
Lakini watu wanahoji kuwa kulitumia neno "Nafri" kama kisawe cha watu waliozuwia kwenye msako ni sawa na kusema kuwa Waafrika Kaskazini wote ni wahalifu.
"Hii si lugha rasmi au istilahi rasmi tunayotumia," alisema msemaji wa wizara ya mambo ya ndani ya Ujerumani, baada ya polisi kukosolewa vikali kwa kutumia neno hilo.
Mkuu wa polisi wa Cologne, Juergen Mathies, alisema pia kwamba anasikitishwa na matumizi ya neno hilo kwenye ujumbe wa Twitter wa polisi, lakini akatetea hatua iliyochukuliwa katika kuhakikisha ya mwaka 2016 hayajirejei kwenye mkesha wa Mwaka 2017.
Wakati kiongozi wa Chama cha Kijani, Simone Peter, akiwakosoa polisi kwa kuwatambulisha Waafrika Kaskazini kama Nafri, wanachama kadhaa wa muungano wa Kansela Angela Merkel waliiunga mkono polisi ya Cologne.