Ni msimamo wa pamoja
21 Julai 2011Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, na rais wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy, wamekubaliana kuwa na msimamo wa pamoja kuhusu mzozo wa madeni wa Ugiriki, huku mkutano wa dharura wa eneo linaloitumia sarafu ya euro ukitarajiwa kufanyika hii leo.
Msemaji wa Merkel alikataa kufichuwa yaliyomo kwenye mpango huo, lakini alisema kuwa viongozi hao wawili walifikia mtazamo wa pamoja kuhusu mzozo huo wa madeni pamoja na benki kuu ya Ulaya na rais wa Umoja wa Ulaya, Herman Van Rompuy mapema hii leo, baada ya mazungumzo ya jana usiku.
Ugiriki inahitaji kiasi ya euro bilioni 110 zaidi, kuimarisha fedha zake hadi mwishoni mwa mwaka 2014. Rais wa baraza la Umoja huo, Jose Manuel Barroso, amesema ni lazima suluhu ya uhakika ipatikane hii leo, la sivyo alionya kuwa uchumi duniani utaathirika.
Masoko yana wasiwasi kuwa Ugiriki ikishindwa kulipa madeni yake, itazusha athari katika nchi nyengine zinazoitumia sarafu hiyo ya euro, ambayo itaziathiri pia nchi zenye uchumi thabiti Ulaya.
Mwandishi:Maryam.Abdalla/ afp, reuters, dpa
Mhariri:Yusuf, Saumu