SiasaNicaragua
Nicaragua yawachia huru wapinzani 222 na kuwapeleka Marekani
10 Februari 2023Matangazo
Wanasiasa hao hata hivyo wamevuliwa uraia wa Nicaragua na kupokonywa haki zote za kisiasa kwenye taifa hilo la Amerika ya Kusini.
Uamuzi huo wa kuwaachia wanasiasa hao 222 ulitangazwa ghafla na utawala wa rais Daniel Ortega wa Nicaragua ambaye analaumiwa kwa kuitumbukiza nchi hiyo kwenye mkondo wa udikteta.
Inaarifiwa uamuzi huo umefikiwa baada ya mazungumzo kati ya serikali ya Nicaragua na Marekani ambapo Washington imeridhia kuwapokea wanasiasa hao na imesema itawahudumia kwa muda wa miaka miwili.
Miongoni mwao ni Juan Sebastian Chamorro aliyetarajiwa kuchuana na rais Ortega katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2021.
Kabla ya uchaguzi huo yeye na wenzake kadhaa walikamatwa na kuwekwa kizuizini kwenye gereza lenye ulinzi mkali.