Nigeria na Ujerumani zatia saini makubaliano ya gesi
22 Novemba 2023Kwa upande wake, Ujerumani itaongeza uwekezaji wa hadi dola milioni 500 katika sekta ya teknolojia na miradi ya nishati mbadala nchini Nigeria.
Katika mkataba wa maelewano uliotiwa saini na kampuni ya Nigeria inayohusika na mradi wa gesi asilia ya Riverside na inayofanya kazi katika jimbo la Delta na kampuni ya kawi ya Ujerumani, Nigeria itasafirisha tani 850,000 za gesi asilia kila mwaka nchini Ujerumani, na baadaye kiwango hicho kitaongezeka hadi tani milioni 1.2.
Usafirishaji wa kwanza ambao utawakilisha asilimia 2 ya gesi asilia kutoka Nigeria kwenda Ujerumani, unatarajiwa kuanza mwaka 2026.
Mwenyekiti wa kampuni hiyo ya kawi ya Ujerumani Jonannes Schuetze amesema makubaliano hayo ni hatua muhimu kuelekea upatikanaji wa gesi zaidi nchini Ujerumani.
Ujerumani ni mwenyeji wa kongamano la wawekezaji mjini Berlin chini ya mpango wa ushirikiano wa mataifa yaliyoendelea kiviwanda ya kundi la G20 na bara la Afrika.
Tangu aingie madarakani mnamo mwezi Mei, Rais wa Nigeria Bola Tinubu amekuwa akijitahidi kuvutia wawekezaji wa kigeni nchini Nigeria ambayo ndio nchi yenye uchumi mkubwa zaidi barani Afrika.