Nyambizi yapotea baharini ikipeleka watalii kuiona Titanic
21 Juni 2023Meli za vikosi vya ulinzi wa pwani vya Marekani na Canada pamoja na ndege zinatafuta eneo la bahari lenye ukubwa wa kilomita 20,000 za mraba, kujaribu kuipata nyambizi hiyo, ambayo ilikuwa inajaribu kuzama chini ya bahari umbali wa maili 400 nje ya pwani ya Newfoundland, nchini Canada.
Kikosi cha ulinzi wa pwani cha Marekani kimesema kupitia ukurasa wake wa twitter kwamba ndege ya P-3 ya Canada iligundua kelele za chini ya bahari katika eneo la utafutaji, na hivyo kuhamisha operesheni katika juhudi za kubaini chimbuko la kelele hizo.
Juhudi za utafutaji mpaka sasa hazijazaa matunda yoyote, lakini kikosi hicho cha ulinzi wa pwani kimesema zitaendelea, na kuongeza kuwa data kutoka ndege ya Canada zimetolewa kwa wataalamu wa jeshi la majini la Marekani kusaidia katika mipango ya baadae ya utafutaji.
Waziri Mkuu wa Newfoundland na Labrador, Andrew Furey, ameyaelezea mazingira ya operesheni ya uokoaji kuwa magumu, akitoa sababu za hali ya hewa. "Tunazungumzia mawimbi yenye urefu wa futi 12, ukungu mzito. Hali ngumu sana ya utafutaji na uokoaji."
soma pia: Merkel ahofia Trump anavyoyavuruga mahusiano ya Bahari ya Atlantiki
Katika majanga ya chini ya bahari, watu waliomo kwenye chombo wasioweza kuwasiliana na walio nje hugonga kwenye fremu ya chombo ili waweze kugunduliwa na kipokezi cha sauti za chini ya bahari, maarufu Sonar.
Hata hivyo mpaka sasa hakuna afisa yeyote aliyesema hali ndivyo ilivyo na kelele za chini ya maji zinaweza kutoka katika vyanzo mbalimbali.
Muda wa kuishiwa hewa ya oksijeni wayoyoma
Nyambizi hiyo iliyotoweka yenye jina la Titan, inayomilikiwa na kampuni ya usafirishaji ya OceanGate ya nchini Marekani, ilijengwa kukaa chini ya maji kwa saa 96, kulingana na maelezo yake - hii ikimaanisha kwamba watu watano waliomo - ambao ni rubani na abiria wanne, wana muda wa hadi kesho asubuhi kabla ya kuishiwa hewa ya oksijeni.
Masalia ya meli ya Titanic, ambayo iliyozama katika safari yake ya kwanza Aprili 1912, yako karibu kilomita 1,450, sawa na maili 900 mashariki mwa Cape Cod, jimbo la Massachusetts, na kilomita 644, sawa na maili 400 kusini mwa Newfoundland.
Watu waliomo kwenye nyambizi ya Titan kwa ajili ya safari hiyo inayogharimu dola za Marekani 250,000 kwa kila mtu, wanaaminika kuwa bilionea wa Uingereza Harmish Harding mwenye umri wa miaka 58, mfanya biashara wa Pakistan Shahzada Dawood mwenye umri wa miaka 48 pamoja na mtoto wake wa kiume Suleman, ambao ni raia wa Uingereza, mgunduzi wa Ufaransa Paul-Henri Nargeolet mwenye umri wa miaka 77, na Mmarekani Stockton Rush, mwasisi na mtendaji mkuu wa kampuni ya OceanGate Expeditions.
Chanzo: Mashirika