Ombi la Oscar Pistorius kuondoka jela mapema lakataliwa
31 Machi 2023Haya ni kulingana na mamlaka za magereza Afrika Kusini na wakili wa familia ya Steenkamp.
Pistorius alikuwa anakubaliwa kisheria kuwasilisha ombi la msamaha na kuachiwa mapema kutoka jela baada ya kuhudumu nusu ya kifungo chake, jambo alilofanya, ingawa familia ya Steenkamp ilikua inalipinga ombi hilo.
Soma pia: Afisa wa magereza ataka Pistorius apewe kifungo cha nyumbani
Na sasa wakili wa familia hiyo, Tania Koen ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba amepokea simu kutoka katika bodi ya msamaha na kuthibitishiwa taarifa hiyo ingawa amesema bodi hiyo itakutana tena baada ya mwaka mmoja kujadili iwapo inaweza kumsamehe Pistorius.
Idara ya magereza imesema bodi ya msamaha imekuta kuwa Pistorius hajamaliza muda wa chini wa kuwa kifungo unaohitajika ili aachiliwe huru.
Kikao cha kusikiliza ombi hilo la msamaha kilifanyika leo katika jela moja ya viunga vya mji mkuu Pretoria ambako mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 36 anazuiliwa.
Soma pia: Pistorius apatikana na hatia ya mauaji
Wazazi wa Steenkamp, ambao wanapinga kuwachiliwa kwake mapema, wakisema kuwa hawaamini kama mwanariadha huyo wa zamani alisema ukweli kuhusu kilichotokea na hajaonyesha huruma na kujutia kitendo chake, wameukaribisha uamuzi huo.
afp, reuters