Papa Francis abariki Macedonia Kaskazini kujiunga na EU
7 Mei 2019Baada ya ziara ya siku mbili nchini Bulgaria, baba mtakatifu Franscis aliwasili katika mji huo mkuu wa Macedonia Kaskazini kwa ziara ya saa 10 mfululizo na kuwa mtu wa kwanza mashuhuri zaidi kufanya ziara katika nchi hiyo tangu ilipobadilisha jina lake kutoka Macedonia mwezi Januari.
Baba mtakatifu alilakiwa kwa mabango ya rangi ya manjano pamoja na watu walioabiri mabasi kadhaa yaliokuwa na picha ya uso wake ukitabasamu baada ya kuwasili katika taifa hilo dogo la Balkan ambalo waumini wake wengi ni wa dhehebu la kikristo la Orthodox. Kanisa Katoliki lina waumini chini ya asilimia moja katika idadi ya watu milioni 2.1.
Akiwahutubia maafisa wakuu wa serikali katika ikulu ya rais ya Skopje, baba mtakatifu Francis alipongeza kile alichokitaja kuwa mchanganyiko wa tamaduni na dini ambazo huenda zikawa mfano kwa wengine. Aliongeza kusema kuwa hali hizo ni muhimu kwa utangamano wa mataifa ya bara Ulaya na ni imani yake kwamba utangamano huu utawezesha kuimarika katika njia ambayo itakuwa ya manufaa kwa eneo zima kwa ujumla.
Wengi wa waliohudhuria walikuwa na hisia tofauti huku baadhi wakilitaja tukio hilo kuwa la kihistoria.
Kabla ya kufanya ibada, baba mtakatifu Francis alikutana na maskini na viongozi wa kidini katika hafla ya kumbukumbu kwa heshima ya mama Teresa ambaye alikuwa mzaliwa wa mji huo. Katika hotuba yake, baba mtakatifu alimpongeza mama Teresa aliyemtawaza mnamo mwaka 2016 kwa kufanya upendo kwa jirani kuwa sheria kuu maishani mwake.
Ijapokuwa mtawa huyo aliishi maisha yake kuwahudumia maskini katika mji wa Calcutta, mfano wake bado unadhihirika katika nchi yake ya kuzaliwa kwa mifano ya sanamu, maeneo ya kumbukumbu na barabara iliyopewa jina lake.
Mataifa sita ya Balkan Magharibi ambayo ni Albania, Bosnia, Kosovo, Montenegro, Macedonia Kaskaini na Serbia wako katika viwango mbali mbali vya kujiunga na Umoja wa Ulaya. Lakini katika taarifa yake, rais wa Macedonia Gjorge Ivanov, alilalamika sana kuhusu kucheleweshwa kwa hatua hizo.
Rais Ivanov alimwambia baba mtakatifu kuwa ziara yake imejiri wakati ambapo jamii ya Macedonia imegawanyika na taifa kutatanishwa kutoka na ahadi ambazo hazijatimizwa, matarajio ambayo hayajaafikiwa na ukosefu wa imani kwa jamii ya kimataifa.
Skopje alikuwa amenuia kujiunga na uwanachama wa NATO na Umoja wa Ulaya tangu kukamilika kwa maandamano ya jamii ya waclio wachache ya Albania lakini ikazuiwa na Ugiriki iliyosisitiza kuwa jina la Macedonia lilimaanisha madai ya umiliki wa ngome yake katika mkoa wa Kaskazini wa nchi hiyo.
Karibu ziara yote ya baba mtakatifu huko Skopje itazingatia kuhusu mama Teresa aliyezaliwa na kuitwa Anjeze Gonxhe Bojahiu ambaye wazazi wake walikuwa raia wa Albania mnamo mwaka 1910.
AFPE; REUTERS