Papa Francis amaliza ziara yake nchini Msumbiji
6 Septemba 2019Papa Francis aliimaliza ziara yake katika nchi hiyo ya Kusini mwa Afrika kwa kuitembelea hospitali ambako akina mama wenye virusi vya UKIMWI wanapatiwa matibabu na kisha alikwenda kwenye uwanja wa michezo wa mjini Maputo ambako aliongoza misa iliyohuhduriwa na waumini wapatao alfu 60.
Watu hao walivumilia mvua na upepo ili kumsikiliza kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki katika uwanja wa Zimpeto huku wakiimba na kucheza wakipeperusha bendera zilizokuwa na sura Papa Francis. Karibu asilimia 28 ya wakazi wapatao milioni 30 wa Msumbiji,koloni la zamani la Ureno ni Wakatoliki.
Papa Francis amewasihi watu wa Msumbiji kuendelea kufuata njia ya maridhiano baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe. Lakini pia amewaonya juu ya hatari ya ufisadi na uvunjifu wa haki unaotendeka wakati maafisa wa umma wanapodai kuwasaidia maskini lakini mara nyingi wanajali zaidi masilahi yao binafsi.
Papa Francis amesema watu wote wana haki ya kuishi kwa amani. Hapo jana alifanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi. Rais wa Msumbiji amemwahidi baba Mtakatifu kuwa utauzingatia wajibu wake kwa moyo wote kwa lengo la kuwaleta pamoja watu wote wa nchi yake na kujenga mazingira ya amani.Msumbiji inatarajiwa kufanya uchaguzi wiki ijayo katika muktadha wa hali ya mvutano na wasi wasi mkubwa juu ya kuzuka tena kwa mapigano.
Baada ya Msumbiji Papa Francis atafanya ziara nchini Mauritius na Madagascar nchi zinazotishiwa na mabadiliko ya tabia nchi. Kongozi huyo wa Kanisa Katoliki analipa kipaumbele suala la mabadiliko ya hali ya hewa.
Vanzo:/DPA/AFP